1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya ulawiti wazidi kakazini mwa Kenya: KNCHR

23 Februari 2023

Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya KNCHR imefichuwa kuwa kuna ongezeko la visa vya ulawiti katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4Ns4y
Jahresrückblick 2020 | Leben hinter Plastik | Kenia, Nairobi
Picha: Donwilson Odhiambo/Zuma/picture alliance

Tume hiyo ya haki za binadamu imeelezea wasiwasi wake kuhusu dhuluma dhidi ya Watoto wadogo ikilaumu mila potofu kwamba inayochangia visa hivyo kuendelea kufanyika vijijini.

Afisa wa tume hiyo Balkheisa Ibrahim, amesema mtoto wa kiume yupo katika hatari kubwa ya kupitia dhuluma ikilinganishwa na mtoto wa kike.

Afisa huyo amesema kwamba,kuna haja ya haki za Watoto kulindwa kikamilifu kwa kiasi kikubwa, ili kuzuia visa vya ulawiti na ubakaji kuripotiwa. "Siku hizi Watoto vijana wanalengwa sana ikilinganishwa na Watoto wa kike. Vijana sawa na watoto wa kike pia wana haki zao..”

Aidha, Bi Ibrahim amesikitika kwamba,baadhi ya wazee wamekuwa wakihusika kutatua kesi za ulawiti nje ya mahakama akisema hilo pia limechangia visa hivyo kuongezeka.

Afisa huyo kadhalika, amehoji kuwa baadhi ya kesi za dhuluma za kijinsia hukosa kuendelea kutokana na mwingiliano wa maafisa wa polisi au afisi ya mkurugezi wa mashtaka ya umma kutokana na madai ya rushwa au sababu za kibinafsi. "Kutokana na tathmini yetu,mwingiliano hufanyika kabla ya kesi haijaripotiwa au wakati kesi imeripotiwa kwa polisi.watu wengine wanatumia ripoti hiyo kama mbinu ya kujifaidisha.Wanasema ili kesi iondolewa, wapewe kiasi Fulani cha pesa”

Mwenyekiti wa wanaharakati katika jimbo hili Mohammed Hassan,amesema kuwa,wakati umewadia kwa idara ya mahakama kuhakikisha jimbo la Marsabit linakuwa na mahakama ya kushugulikia masuala ya Watoto akisema hilo litasaidia katika kupambana na uovu wa ulawiti na ubakaji. "Tunaomba idara ya mahakama itupoe mahakama moja itakayoshugulika masula ya Watoto kama ilivyo katika maeneo mengine ya taifa ili visa vya kijinsia vishugulikiwe”

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita,visa vinane vya ulawiti viliripotiwa katika eneo la kaskazini mwa taifa japo tume ya kitaifa ya kuteta haki za binadamu inasema kuwa huenda visa hivyo ni vingi ila haviripotiwi kila mara.

Michael Kwena, DW Marsabit