1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipi kuushinda uharamia wa meli huko Somalia?

Miraji Othman11 Desemba 2008

Suluhisho kwa uharamia wa meli huko Somalia

https://p.dw.com/p/GDvg
Maharamia wakiishikilia meli ya Ukraine, FAINA, katika mwambao wa SomaliaPicha: AP

Andrew Mwangura ni mtu jasiri, na hivi sasa ni mtu anayetakiwa sana kuhojiwa na vyombo vya habari, kama bingwa wa masuala ya uharamia wa meli. Si muda mrefu uliopita alikamatwa na wakuu wa usalama wa Kenya, kwa vile hadharani alielezea wasiwasi kama vile vifaru vya kijeshi viliovokuwemo ndani ya ile meli ya Ukraine iliotekwa nyara katika mwambao wa Somalia vilikuwa kweli kwa ajili ya jeshi la Kenya na sio, kama vile ilivochukuliwana watu wengu, kwamba vilikusudiwa kwenda Kusini mwa Sudan.

Na vipi mkasa huo unahusiana na uamuzi wa jana wa baraza la mawaziri la Ujerumani mwishowe kulipa uwezi jeshi la maji la nchi hii kutumia nguvu za kijeshi katika kuwasaka maharamia wa meli katika mwambao wa Afrika Mashariki?

Jana hiyo hiyo Andrew Mwangura alisema jambo la ujasiri zaidi, nalo ni kwamba inahitaji zaidi kuliko manuwari za kivita kulimaliza balaa hili la maharamia wa meli katika mwambao wa Somalia. Hivyo, mwananchi huyo wa Kenya alitia chumvi kwenye kidonda, yeye ni mtu anayetokea nchi jirani na Somalia, yaani Kenya, ilioumia sana kutokana na michafuko ya huko Somalia. Bila ya shaka, mlolongo huo wa manuwari za ile Operesheni ilioanzishwa na Marekani, kwa jina la Operation Enduring Freedom, zile za Jumuiya ya Kujihami ya NATO na za kitaifa unaweza kuwafukuza maharamia hao. Ikiwa sasa shehena za misaada kwa Somalia mwishowe zitaweza kuwasili tena katika bandari ya Mombasa, bila ya shaka, hilo litakuwa ni fanikio. Lakini hiyo sio kwamba tatizo litaondoka. Maharamia hao zaidi wanahamishia vituo vyao vya operesheni upande wa kusini. Huko, kwa mfano, kikosi cha Ujerumani kwa sasa hakitakiwi kupiga doria.

Mazungumzo ya sasa kuhusu uharamia wa baharini yamechomoza kwa muda mfupi sana, na, kwa sehemu, yanachukuwa sura ya ajabu. Kwa mfano, jumuiya ya wamiliki wa meli wanataka manuwari za Kijerumani ziwe tayari kuisindikize kila meli ya abiria. Na jee, vipi, baadae itakuwa watungaji shabaha wa Kijerumani wawasindikize watalii wa mazingira huko Afghanistan ya Kaskazini`?

Kile inachohitaji Somalia sio kila wakati vikosi vipya vya manuwari katika mwambao wake na sio mikutano ya kupambana na maharamia, kama inavofanyika sasa huko Nairobi. Kile inachohitaji nchi hiyo ni suluhisho jumla la kisiasa, suluhisho ambalo litatilia maanani ukubwa ulio wazi ambao mzozo huo wa Somalia umechukuwa katika mkoa huo.

Bila ya shaka, wanasiasa wa Kisomali na wababe wa kivita wa nchi hiyo ambao tangu mwaka 1991 wameirejesha nyuma nchi hiyo katika enzi za kale, wako mbele kubeba dhamana. Hasa Rais Abdullahi Yussuf. mbabe wa kivita asiyekuwa na sifa nzuri, mtu ambaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linamn'gan'gania, bila ya msingi.

Hata hivyo, jamii ya kimataifa inabeba lawama pia. Tangu ile operesheni ilioongozwa na Wamarekani, ilioshindwa mwanzoni mwa miaka ya tisini, na kupewa jina la Kurejesha Matumaini katika Somalia, jamii ya kimataifa, chini ya uongozi wa Wamarekani wanaosmbuka bado na kushindwa huko, haijatunga tena siasa madhubuti kuelekea Somalia au kuelekea Pembe ya Afrika. Makosa yaliofanyika, kama vile Marekani kuuunga mkono Muungano wa ajabu wa wababe wa kivita au kuvishambulia bila ya kuchaguwa vijiji vya Wasomali, vimeifanya itikisike imani ya Wasomali juu ya mfumo wa suluhisho wa kutoka nchi za Magharibi.

Na zaidi, kuna jambo moja katika mazungumzo haya ya sasa ambalo linaachwa kabisa. Ni meli za uvuvi za Warussia, Wachina na Wa-Spain ambazo zinavuwa kiholela katika pwani ya Somalia yenye samaki, hivyo kuwapokonya wavuvi wa Kisomali msingi wa hali yao ya kimaisha.

Marekani wiki ijayo inataka kuwasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio kuhusu mada ya uharamia wa baharini. Hilo ni jambo la kupongzwa, lakini inaponya tu alama za mzozo wa Somalia. Ingekuwa bora kwa Marekani, kama ilivofanya Jumuiya ya kimkoa ya nchi za Pembe ya Afrika, IGAD, kuipa wakati wa mwisho serekali ya mpito ya Somalia isiofanya kazi vizuri, na kuilazimisha iziingize pande zote katika mwenendo wa kutafuta amani ya nchi hiyo. Mpango wa amani wa karibuni uliofikiwa huko Jibuti, licha ya makosa yake yote, unaweza kuwa ni msingi wa mwenendo huo wa kutafuta amani.