1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa zamani zaidi ya 100 wapigania kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa Myanmar

3 Desemba 2008

wamtaka Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa aelekee nchini humo kutoa shinikizo.

https://p.dw.com/p/G8Cf
Kiongozi wa upinzani na mpigania demokrasia nchini Myanmar Bibi Aung San Suu Kyi.Picha: AP

Zaidi ya viongozi 100 wa zamani wa taifa na serikali wamemuandikia barua katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon wakimtaka asafiri kwenda Myanmar ili kuwashinikiza watawala wa kijeshi nchini humo kumuachia huru kiongozi wa upinzani anayepigania demokrasia Bibi Aung San Suu Kyi pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa.

Viongozi hao ni pamoja na marais wa zamani wa Marekani George Bush baba wa rais wa sasa George W.Bush, na Jimmy Carter, Rais wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachov, Waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa Lionel Jospin na mwenzake wa Australia John Howard, Waziri mkuu wa zamani wa Japan Junichiro Koizumi na marais wa zamani wa Philippines Fidel Ramos na Bibi Corazon Aquino.

Waziri mkuu wa zamani wa Norway Kjeli Magne Bondevik ambaye sasa ni rais wa taasisi ya amani na haki za binaadamu ambayo pamoja na shirika la haki za binaadamu lenye makao yake makuu nchini Marekani Freedom Now waliongoza kampeni hiyo alisema," Hili ni tukio la aina yake la mshikamano wa kimataifa na umma wa Burma (Myanmar) na ninafuraha kuona wengi wamejiunga nami katika suala hili."

Viongozi hao wa zamani kutoka zaidi ya mataifa 50 walimtaka Bw Ban binafsi kwenda Myanmar kabla ya mwisho wa mwaka huu kupigania kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa 2.100 wanaoshikiliwa na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

Mwezi uliopita zaidi ya wanaharakati 100 wakiwemo wanachama wa chama cha Bibi Aung San Suu Kyi, National League for Democracy na wafanyakazi wa shughuli za misaada, waandishi habari, watawa na wanasheria walipewa adhabu kali kila mmoja ya hadi vifungo vya miaka 69 jela. Kufungwa kwao kulitokana na hatua za kuwaandama wale waliohusika na maandamano ya upinzani katikati ya mwaka jana 2007 yaliokandamizwa kinyama na seriakali ya kijeshi.

Barua ya viongozi hao wa zamani duniani imekumbusha kwamba Oktoba 11 mwaka jana baraza la usalama la umoja wa mataifa, lilitoa wito wa kuachiwa mapema wafungwa wa kisiasa nchini Myanmar na umoja wa mataifa ukaliweka suala la kuachiwa wafungwa wa kisiasa kuwa kipa umbele kwa mwaka huu wa 2008.

Tangu uasi wa umma mwaka mmoja uliopita, mjumbe maalum wa katibu mkuu Ban Ki-monn, Ibrahim Gambari ameizuru Myanmar mara nne lakini ameshindwa kufufua mazungumzo kati ya utawala wa kijeshi na Bibi Suu Kyi.

Mawaziri kutoka mataifa matano wanachama wakudumu wa baraza la usalama, Marekani ,Uingereza, Ufaransa, Urusi na China pamoja na wa nchi nyengine wakiwemo majirani wa Myanmar wanachama wa Jumuiya ya kusini mashariki mwa Asia-Indonesia , Singapore, Vietnam na Thailand walikutana kandoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa mjini New York mwezi Septemba na kuutaka utawala wa kijeshi wa Myanmar uchukue hatua kuleta mageuzi ya kisiasa kabla ya ziara ya katibu mkuu kabla ya mwisho wa mwaka huu. Lakini hadi sasa wito wao unaelekea umegonga mwamba masikioni mwa watawala hao mjini Yangoon.