1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa IAAF walijua kuhusu rushwa

15 Januari 2016

Mchezo maarufu ambao ni nguzo muhimu katika michezo ya Olimpiki unaendelea kukumbwa na kashfa inayoonekana kuupaka tope. Ripoti ya WADA imewatuhumu viongozi wa IAAF

https://p.dw.com/p/1HeLC
Dick Pound
Picha: Reuters/M. Dalder

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu – WADA umegundua kuwa Shirikisho la Riadha Ulimwenguni – IAAF lina uozo wa ndani wa rushwa kutoka kwa “kikundi cha matapeli chenye nguvu” kikiongozwa na rais wake na walishirikiana kuwatapeli wanariadha na kuwaruhusu Warusi kuendelea kushiriki mashindanoni licha ya vipimo vya damu kugundulika kuwa walitumia dawa hizo.

Ripoti ya jopo la WADA ilisema pia Viongozi wengine wa IAAF wana makosa kwa sababu lazima walifahamu upendeleo ambao ulimruhusu Lamine Diack kuigeuza IAAF kuwa chama chake cha kibinafsi wakati wa uongozi wake wa miaka 16 kama rais. Rais wa zamani wa WADA Dick Pound alisema ni wazi kuwa wafanyakazi wa IAAF walifahamu kuhusu matatizo ambayo yalijitokeza. Amesema "Ilikuwa dhahiri kwa tume kuwa ufahamu wa kitaasisi na matatizo ya Urusi ulikuwa mpana sana kuliko ilivyotambulika, na IAAF haijaonyesha azma halisi ya kuyashughulikia matatizo hayo".

Sebastian Coe Lamine Diack IAAF LOC Peking Weltmeisterschaft
Rais wa IAAF Sebastian Coe na mtangulizi wake Lamine DiackPicha: picture-alliance/dpa/F.Robichon

Ripoti hiyo ilisema kuwa Sebastian Coe ambaye alichukua uongozi kutoka kwa Diack, hakujihusisha katika matukio yoyote ya rushwa, lakini kama makamu wa rais chini ya Diack alikuwa sehemu ya baraza la shirikisho hilo ambalo limekosolewa vikali. Ni kauli anayoiunga mkono bingwa wa zamani wa Kenya Moses Kiptatui aliyemkosoa Coe kwa kutofanya vya kutosha katika kufichua rushwa lakini anasema kitu muhimu sasa ni uongozi wa IAAF kufanya juu chini na kuisafisha sura ya riadha. "Nimesikia vitu kadhaa kuhusu Sebastian Coe, kuhusu Sergei Bupka, nimesikia vitu vingi, lakini kwangu havinihusu kwa sababu nataka tu wawe na moyo wa kiutu katika riadha, ili tuimarishe mchezo huo. Wanaweza pia kutubu na kusalia hapo ili kuyarekebisha mambo na kuwaruhusu wanariadha hawa na kila mtu awaunge mkono ili uonekane kama mchezo wa kweli.

Coe hata hivyo alijitetea akisisitiza kuwa muhimu sasa ni kuweka mikakati mipya ya kuleta mageuzi katika IAAF. Amesema "ndiyo. Baraza la IAAF lilipaswa kufahamu zaidi kuhusu yaliyotokea. Je lilikuwa katika hali ya kujua zaidi? Hapana. Na nnahitaji kuweka mifumo itakayohakikisha kuwa baraza la sasa na litakalolirithi na mrithi wangu hatakuwa katika hali ambayo hatufahamu namna mambo yanavyoendeshwa kila siku katika shirika hili"

Kenya ilikuwa na hofu kubwa kuwa huenda ikaadhibiwa na IAAF kama ilivyofanywa kwa Urusi, na hivyo kuyaathiri maandilizi ya nchi hiyo ya kushiriki katika michezo ya olimpiki mwezi Agosti. Lakini akizungumza baada ya kutolewa ripoti ya WADA, waziri wa michezo wa Kenya, Hassan Wario alisema shirika la kitaifa la kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni – ADAK linashirikiana kwa karibu na IAAF ili kuwalinda wanariadha safi na kuwaadhibu wanaopatikana na hatia. Wario Amesema serikali itaimarisha juhudi zake za kupambana na tabia hiyo mbovu ambayo inaichafua sifa ya Kenya katika ulimwengu wa riadha

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Gakuba Daniel