Viongozi wa dunia kuhutubia baraza kuu la umoja wa mataifa
24 Septemba 2012Maneno ya tahadhari pamoja na ukaidi yanatarajiwa wakati rais wa Marekani Barack Obama , kiongozi wa Iran Mahmoud Ahmedinejad na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu watakapojiunga na zaidi ya viongozi 120 wa mataifa na serikali katika baraza kuu la umoja wa mataifa.
Kwa sababu ya mgawanyiko mkubwa wa kimataifa kuhusiana na mzozo uliodumu sasa miezi 18 nchini Syria , umoja wa mataifa hautakuwa na mkutano rasmi kuhusiana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.
Obama kuhutubia kwanza
Lakini rais Obama na viongozi wa mataifa ya magharibi wanatarajiwa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua katika hotuba zao. Rais wa Marekani ni mmoja kati ya wazungumzaji wa mwanzo siku ya Jumanne asubuhi baada ya tukio hilo kufunguliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon.
Na kampeni dhidi ya Syria itaendelezwa nje ya baraza kuu la umoja wa mataifa. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Kiarabu, Arab League Lakhdar Brahimi atatoa maelezo katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kesho Jumatatu kuhusiana na mazungumzo yake na rais Bashar al-Assad.
Syria pia inakuwa mada kuu katika baraza la usalama wakati wa mjadala wa mawaziri kuhusiana na Arab League siku ya Jumatano, umoja wa ulaya unatarajiwa kuanzisha wito mpya kwa ajili ya mfuko wa fedha za huduma ya kiutu na mkutano wa mawaziri wa marafiki wa Syria unapangwa kufanyika siku ya Ijumaa.
Majeraha ya kidiplomasia
Majeraha ya kidiplomasia kuhusu Syria hayako karibu na kupata nafuu. Si Urusi ama China , nchi ambazo zimetumia kura zao za turufu mara tatu kuzuwia maazimio ya baraza la usalama kuhusu Syria , zitawakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu mjini New York.
Assad anatarajiwa kumtuma waziri wake wa mambo ya kigeni.
"Kila mmoja atakuwa anafikiri kuhusu Syria, atazungumza kuhusu Syria , lakini hakutakuwa na uamuzi na hakuna hatua kubwa itakayopigwa," amesema mwanadiplomasia mmoja mwandamizi wa umoja wa mataifa, akizungumza kwa mashariti ya kutotajwa jina.
Stewart Patrick , mtaalamu wa taasisi ya kimataifa inayokusanya mawazo kuhusu utawala wa dunia kwa ajili ya baraza la uhusiano wa kimataifa , amesema hata hivyo kuwa Syria itakuwa moja ya masuala yanayopewa umbele katika baraza kuu la umoja wa mataifa pamoja na mvutano kuhusu Iran. Ahmedinejad yuko mjini New York huenda kwa mara yake ya mwisho kuonekana katika baraza kuu.
Wasi wasi wazidi
Hali ya wasi wasi wa usalama pamoja na diplomasia zaidi vinatarajiwa huku kukiwa na uvumi mkubwa kuwa Israel inapanga kuishambulia kijeshi Iran katika maeneo yake ya kinuklia ambapo Iran inasisitiza kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya amani, lakini mataifa ya magharibi yanasema nchi hiyo inaficha majaribio ya kutengeneza bomu la nuklia.
Ahmedinejad atazungumza katika baraza kuu siku ya Jumatano, wakati hatua mpya ya mataifa kadha kutoka katika ukumbi huo ikitarajiwa iwapo kiongozi huyo wa Iran atarejea matamshi yake ya kuishambulia Israel.
Maafisa wa ngazi ya juu kutoka Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani , ambao wanajaribu kujadiliana na Iran, wanatarajiwa kukutana siku ya Alhamis mara tu baada ya waziri mkuu wa Israel Netanyahu kulihutubia baraza kuu la umoja wa mataifa.
Obama na Netanyahu
Kushindwa kutayarisha mkutano kati ya Netanyahu na rais Obama kumezusha uvumi kuhusu kuongezeka kwa mpasuko kati ya viongozi hao wawili. Marekani na washirika wake wameongeza juhudi zao za kutoa onyo kwa Iran, hata hivyo , muda unafikia tamati kwa ajili ya kupata suluhisho kuhusiana na mvutano huu.
Netanyahu atahutubia baraza kuu mara baada ya kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas kuhutubia. Mwaka jana kiongozi huyo wa Palestina alikuwa kivutio kikubwa kwa juhudi zake zilizovuta hisia za kutaka kuwa mwanachama kamili wa umoja wa mataifa, juhudi ambazo zimezuiwa na Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo /afpe
Mhariri: Iddi Ismail Ssessanga