1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Syria vyaendeleza mashambulizi dhidi ya wapinzani

Josephat Nyiro Charo16 Februari 2012

Vikosi vya Syria vimeushambulia mji wa Deraa hii leo katika juhudi za kujaribu kuwachakaza wanajeshi walioasi katika mji huo ambamo upinzani dhidi ya rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, ulianza Machi mwaka jana.

https://p.dw.com/p/143zL
epa03105393 An undated handout photograph made available by the Local Coordination Committees (LCC) in Syria on 13 February 2012, shows smoke rising near a mosque reportedly following shelling by the Syrian army in the Bab Amr neighborhood of Homs, Syria. Syrian security forces intensified 14 February their attacks on rebel areas in the northern and the southern parts of the country, killing at least three people and arresting dozens, activists said. The onslaught came just a day after UN High Commissioner for Human Rights Navi Pillay told the UN General Assembly that President Bashar al-Assad was behind "crimes against humanity." In Homs, shells rained down on the neighborhood of Baba Amr, hitting a civilian car and killing three of its passengers, Omar Homsi, an activist based in al-Qusayr told dpa by satellite phone. EPA/LOCAL COORDINATION COMMITTEES LCC / HANDOUT BEST QUALITY AVAILABLE. EPA IS USING AN IMAGE FORM AN ALTERNATIVE SOURCE, THEREFORE EPA COULD NOT CONFIRM THE EXACT DATE AND SOURCE OF THE IMAGE pixel
Mashambulio yaendelea SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Watu wasiopungua wanne wameuwawa wakati wanajeshi wa Syria wakisaidiwa na magari ya deraya walipoushambulia mji wa Deraa kwa mabomu alfajiri ya leo. Kwa mujibu wa wakaazi na wanaharakati wa upinzani, milio ya milipuko na bunduki za rashasha imesikika katika vitongoji vya al-Balad, al-Mahatta na al-Sad vya mji huo ulioko katika mpaka na Jordan, huku vikosi vya serikali vikiwashambulia waasi.

Marekani imepuuzilia mbali ahadi ya kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini Syria, ikiitaja kuwa kichekesho. Msemaji wa ikulu ya Marekani, Jay Carney, amesema ahadi hiyo inakejeli mapinduzi nchini Syria. Msemaji huyo pia amesema ahadi za mageuzi zimekuwa zikifuatiwa na ongezeko la machafuko na hazijawahi kutimizwa na utawala wa Syria, tangu kuanza kwa maandamano ya amani nchini humo.

Hapo jana rais wa Syria, Bashar al Assad, kwa haraka aliamuru kura ya maoni ifanyike wiki mbili zijazo kuhusu pendekezo la katiba mpya itakayoviruhusu vyama vya kisiasa mbali na chama cha Baath, kushiriki katika chaguzi. Upinzani wa Syria umeipinga vikali hatua hiyo na kuwataka Wasyria waikatae na kuigomea kura hiyo ya maoni.

Akizungumza jana akiwa ziarani nchini Brazil, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema mapendekezo yote ya rais Assad yatachunguzwa kwa makini, lakini mbinu za kijanja anazozitumia hazitakubalika.

Germany?s Foreign Minister Guido Westerwelle speaks during a press conference at Itamaraty palace in Brasilia, Brazil, Monday Feb. 13, 2012. Westerwelle is on a three-day visit to Brazil. (Foto:Eraldo Peres/AP/dapd)
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa BrazilPicha: dapd

"Cha muhimu kwetu ni njia iwekwe wazi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kidemokrasia na machafuko yakomeshwe. Machafuko yanafanywa na utawala wa Assad. Anabeba dhamana na lazima ang'atuke."

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuijadili Syria

Wakati huo huo, baraza kuu la Umoja wa Mataifa linakutana leo kujadili pendekezo la azimio lililoandaliwa chini ya uongozi wa Saudi Arabia, linalolaani machafuko yanayoendelea Syria na linalotaka mageuzi ya kisiasa kuelekea mfumo wa demokrasia.

Azimio hilo linajumuisha lugha iliyotumika katika azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililopingwa na Urusi na China kutumia kura zao za turufu mnamo tarehe 14 mwezi huu. Hakuna mamlaka ya kura ya turufu katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo nchi 193 wanachama zina kura sawa.

Iwapo baraza kuu litaridhia azimio hilo, itakuwa mara ya pili tangu Desemba mwaka jana kwa baraza hilo kulaani ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria.

Kwa upande mwingine, Uswisi imesema itaufunga ubalozi wake mjini Damascus na imewataka raia wake waondoke Syria haraka iwezekanavyo. Uswisi ilimuondoa balozi wake kutoka Syria baada ya kuanza kwa ukandamizaji, lakini iliuacha wazi ubalozi wake ili kuwasaidia raia wake kati ya 150 na 180 wanaoishi nchini humo, wengi wao wakiwa na uraia wa nchi mbili.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE

Mhariri: Daniel Gakuba