1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya muungano vyateka miji miwili karibu na Mosul

Jane Nyingi
24 Oktoba 2016

Vikosi vya Iraq vimechukua udhibiti wa vijiji viwili vilivyo karibu na mji wa Mosul huku operesheni za kuukomboa mji huo kutoka kwa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS zikiingia wiki yake ya pili

https://p.dw.com/p/2ReQT
Irak kurdische Kämpfer um Mossul
Picha: Reuters/A. Lashkari

Vikosi vya Iraq vimefanikiwa kuchukua udhibiti wa vijiji viwili vilivyo karibu na mji wa Mosul huku operesheni za kuukomboa mji huo kutoka kwa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS zikiingia wiki yake ya pili. Hayo yanajiri huku ukiendelea mvutano kati ya Uturuki na Iraq baada ya Uturuki kudai ni muhusika katika operesheni hiyo ya kuwaondoa IS Mosul suala lililopingwa vikali na waziri mkuu wa Iraq.

Uturuki imepuuza agizo la Iraq la kuyaondoa majeshi yake karibu 500 yanayotoa mafunzo kwa vikosi vya kisunni na kikurdi kaskazini mwa mji huo,ikisema ina ruhusa ya kuendesha shughuli zake.Waziri wa maswala ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema tangu kuanza operesheni hiyo ya kuukomboa mji wa Mosul vikosi vya Uturuki vimewaua wapiganaji 17 wa IS.

Iran yataka vikosi vya Uturuki kuondoka Iraq

Waziri huyo amesema ndege za kivita za Uturuki ni sehemu ya muungano wa vikosi vinavyongozwa na Marekani; madai yaliyotajwa na waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi kuwa ya uongo na kuvitaka vikosi vya Uturuki kwa mara nyingine kuondoka Iraq. Rais wa Iran Hassan Rouhani pia amejitosa katika mzozo huo na kusema Uturuki inapaswa kupata ruhusa kutoka kwa serikali ya Iraq ili kushiriki katika operesheni hiyo ya kukabiliana na IS "Tunachukulia uingiliaji wa mataifa ya kigeni nchini Iraq na Syria chini ya kisingizio cha kupambana na ugaidi, na bila kuwasiliana na nchi mwenyeji, kuwa jambo hatari sana, hata ikiwa ni vikosi vya kivita, vya mashambulizi ya angani au ardhini ."

New York UN iranischer Präsident Hassan Rouhani
Rais wa Iran Hassan Rouhani Picha: picture-alliance/newscom/M. Graff

Katika operesheni ya Leo(24.10.2016) vikosi maalum vya Iraq vimefanya mashambulizi ya mabomu karibu na mji wa Bartella,ambao kihistoria ulikuwa ukikaliwa na wakristo.Kisha baadae vikosi hivyo chini ya makabiliano makali vilifanikiwa kusonga mbele hadi kijiji cha Tob Zawa kilicho karibu kilomita 9 kutoka mji wa Mosul. Baada ya kuingia kijiji hicho, waliwaruhusu kuondoka zaidi ya watu 30 ambao walikuwa wametafuta hifadhi katika shule baada ya kutoroka mapigano. Muungano wa vikosi vinavyoongozwa na Marekani umefanikiwa kufanya mashambulizi sita ya angani ,na kuharibu kabisa maeneo tisa ya vita ya kundi la IS pamoja na magari yao 17.Taarifa nyingine ni kuwa raia 11 wanaripotiwa kuuawa na wengine 35 kujeruhiwa kufuatia msururu wa mashambulizi madogo ya mabomu mjini Baghdad. Mashambulizi hayo yalilenga magari na maeneo yenye shughuli nyingi. Hakuna aliyejitokeza kukiri kuhusika lakini kundi la IS limekuwa likivishambulia vikosi vya usalama na maeneo yaliyo karibu na washia katika mji huo mkuu.Wapiganaji hao wa IS katika siku za hivi karibuni wameanzisha mashambulizi mbali kabisa na mstari wa mbele wa mapambano ambao ni mji wa Mosul na kuulenga mji ulio kaskazini wa Kirkuk na ule wa magharibi wa Rutba na upo wasiwasi mkubwa wataulenga pia mji wa Baghdad.

Mji wa Bartella ulio kaskazini mwa Iraq
Mji wa Bartella ulio kaskazini mwa IraqPicha: Mulham Shaalan

Mwandishi:Jane Nyingi /APE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga