Vikosi vya Gbagbo vyaidhibiti tena Abidjan
9 Aprili 2011Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, Alain Le Roy ameonya kuwa vikosi vya Gbagbo bado vina vifaru na silaha nyingine nzito na kwamba wako umbali wa kilometa moja tu kutoka kwenye hoteli ambayo ndio makao makuu ya kiongozi anayetambuliwa kimataifa, Alassane Ouattara.
Gbagbo amekataa kukabidhi madaraka kwa Ouattara tangu uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka uliopita na ameendelea kubakia katika handaki kwenye makaazi yake mjini Abidjan, ambayo yamezingirwa na vikosi vya Ouattara. Mashirika ya kutoa misaada yameonya kuongezeka kwa mzozo wa kibinaadamu nchini humo.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya jana umeondoa vikwazo dhidi ya Cote d'Ivoire, ikiwemo kuzuia bandari mbili muhimu. Ouattara aliutaka umoja huo kuiondolea vikwazo nchi hiyo ambayo ipo katika machafuko kwa lengo la kuirejesha katika hali yake ya kawaida.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP,AP,RTRE)
Mhariri: Halima Nyanza