1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Ethiopia vyaukomboa mji mwingine mkoani Tigray

John Juma
16 Novemba 2020

Jopo la serikali linaloshughulikia masuala ya dharura limesema hayo usiku wa kuamkia Jumatatu, huku likiwashutumu viongozi wa jimbo hilo kwa kuwafungulia wafungwa 10,000 katika mji huo walipokuwa wakikimbia.

https://p.dw.com/p/3lLuI
Äthiopien Amhara-Soldaten auf dem Weg nach Tigray
Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Jopo kazi hilo la serikali limeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba, wakati wapiganaji wa chama kinachotawala katika jimbo la Tigray- TPLF, waliposhindwa katika mji wa Alamata, walitoroka wakiwa pamoja na wafungwa 10,000.

Hata hivyo hapakuwa na kauli ya moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa Tigray kuhusiana na matukio katika mji wa Alamata, mji ulio takriban kilomita 120 mbali na mji mkuu wa Tigray Mekelle lakini ulio karibu na mpaka wa jimbo la Amhara.

Hayo yakijiri, kiongozi wa jimbo hilo linaloasi la Tigray Debretsion Gebremichael, ameuhimiza Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika kuishutumu serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, kwa kutumia silaha za hali ya juu kiteknolojia zikiwemo ndege zisizokuwa na rubani, wakati wa operesheni yake ya kijeshi ambayo imedumu kwa wiki mbili sasa.

Äthiopien Konflikt Tigray | Proteste
Wandamanaji wa Ethiopia wanaopinga mapigano ya TigrayPicha: Million Hailessilasie/DW

Kwenye taarifa, Gebremichael amesema Abiy anaendeleza vita dhidi ya watu wa Tigray na ndiye wa kuwajibika kufuatia dhiki ya makusudi dhidi ya raia pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu kama bwawa la Tekete na kiwanda cha sukari cha Wolkait.

Kumekuwa na maandamano pia ya kulaani machafuko yanayoendelea huku wakitoa miito ya usitishaji vita. 

Mnamo siku ya Jumamosi, vikosi vya Tigray vilifyatua roketi kuelekea nchi jirani ya Eritrea,hivyo kuzidisha machafuko ambayo yamedumu kwa zaidi ya siku 13 sasa.

Mamia ya watu wapoteza maisha

Mgogoro huo tayari umesababisha vifo vya mamia ya watu katika pande zote mbili zinazozozana, hali inayotishia utulivu wa maenero mengine ya Ethiopia.

Kwa kuwa huduma za mawasiliano zimeathiriwa pakubwa katika jimbo hilo la Tigray, shirika la Habari la Reuters ilishindwa kuthibitisha madai yaliyotolewa na pande zote mbili.

Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani barani Afrika Tibor Nagy amelaani mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Tigray kuelekea Eritrea, akiyaita kuwa juhudi za kuchochea machafuko hayo ya Tigray kuwa ya kimataifa.

Rais wa jimbo la Tigray Debretsion Gebremichael ameishutumu Eritrea kwa kutuma vifaru Pamoja na maelfu ya wanajeshi katika jimbo hilo kuunga mkono mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia.

Lakini wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Eritrea Osman Saleh Mohamed aliliambia shirika la Habari la Reuters kwamba nchi yake haijajiingiza katika mzozo huo.

Äthiopien I Proteste in Dire dawa
Maandamano mengine yaliyofanyika katika mji wa Dire dawaPicha: Mesay Tekeli/DW

Mnamo Novemba 4, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya viongozi wa jimbo la Tigray, baada ya kuwatuhumu viongozi hao kwa kuvishambulia vikosi vya serikali kuu walioko katika jimbo hilo la kaskazini linalopakana na Eritrea na Sudan na ambalo pia ni nyumbani kwa watu milioni 5.

Mapigano yalisambaa hadi katika jimbo la Amhara ambalo vikosi vyake vinapigana na vikosi vya serikali kuu katika jimbo la Tigray.

Mnamo Ijumaa usiku, viwanja viwili vya ndege katika jimbo la Amhara, vilishambuliwa kwa roketi. Chama cha TPLF kilisema mashambulizi hayo yalikuwa ulipaji kisasi dhidi ya mashambulizi ya angani yaliyofanywa na vikosi vya serikali. Serikali imesema lengo la mashambulizi yao ni kuharibu vifaa vinavyodhibitiwa na vikosi vya Tigray. Umoja wa Mataifa umesema Waethiopia wasiopungua 20,000 wamekimbia nchi yao kuenda Sudan kwa sababu ya machafuko hayo.