Vigogo vya ligi ya mabingwa vyaendelea kutesa
20 Oktoba 2010Timu za ligi kuu ya Uingereza Arsenal na Chelsea pamoja na Bayern Munich ya Ujerumani na Real Madrid ya Hispania zimeendelea jana usiku kuelekea katika kukata tikiti ya kushiriki katika awamu ya michezo ya mtoano katika ligi ya mabingwa barani Ulaya, Champions League wakati kila moja ilifanikiwa kushinda kwa mara ya tatu katika michezo mitatu hadi sasa ya ligi hiyo ya mabingwa.
Mjini Munich, CFR Cluj wageni wa Bayern Munich kutoka Romania walipachika wavuni mabao manne kati ya matano usiku wa jana , lakini mawili kati ya hayo yalitumbukia katika nyavu zao wakati wenyeji wao Bayern Munich wakishinda pambano hilo kwa mabao 3-2, wakati huo huo Real Madrid iliweka msingi wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya AC Milan katika kipindi cha kwanza cha pambano lao.
Arsenal london ilionyesha kuwa ni mzigo mzito kwa Shakhtar Donetsk, na kuirarua timu hiyo kwa mabao 5-1, wakati Chelsea London nayo ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Spartak Moscow.
Mjini Munich mashabiki 64,000 walishuhudia mlinzi raia wa Ureno Cadu akiwashangaza kwa kupachika bao dhidi ya timu hiyo ya kocha Luis van Gaaal , katika dakika ya 28, lakini dakika nne baadaye aligeuka kutoka kuwa shujaa na kuwa wa kulaumiwa baada ya kuutumbukiwa mpira uliopigwa na Toni Kroos katika nyavu zake.
Bayern ilichukua uongozi wa mchezo huo kwa bao la dakika ya 37 wakati mpira wa kona ulipomgonga Cristian Panin gotini na kuingia wavuni. Mario Gomez aliihakikishia Bayern Munich ushindi wa mchezo huo katika dakika ya 77 wakati Cadu alipojaribu kuuondoa mpira huo, lakini uligonga tena Gomez na kujaa wavuni.
Juan Culio aliufumania mlango wa Bayern zikiwa zimesalia dakika nne mpira kumalizika , lakini ilikuwa bahati mvaya tena kwa wageni hao kutoka Romania kuweza kurejesha mabao yote.
Binafsi Mario Gomez amekiri kuwa goli lake lilikuwa zaidi kama goli la kujifunga wenyewe kuliko juhudi zake. Tunahitaji kuwashuruku Cluj kwa mabao yote matatu. Lakini hii ni soka , wakati mwingine mambo yanakwenda upande wako, amesema Gomez.
Mmeona jinsi ilivyo vigumu kucheza na timu ambayo inacheza kwa kujihami mno, lakini nimefarijika kuwa nafunga magoli na kwamba napata nafasi tena ya kucheza.
Kocha wa Bayern Munich Louis van Gaal amesema kuwa timu yake ilistahili kupata bahati iliyopata. Hatuna bahati msimu huu, kwa hiyo bahati kidogo katika mchezo ni jambo la kufurahisha. Ni vigumu ikiwa timu pinzani inacheza na watu kumi katika ulinzi.Nafikiri wachezaji wetu wa kati wamefanya kazi nzuri. Waliweza kuufanya mpira uzunguke huku na huko na kuwaweka wapinzani wetu katika mbinyo.
Katika mchezo mwingine wa kundi E Basel iliwashangaza AS Roma kwa kuichapa mabao 3-1. Real Madrid ilifanikiwa kupachika mabao 2 kupitia Cristiano Ronaldo na Mesut Özil katika kipindi cha dakika moja katika mchezo wao wa kundi G dhidi ya AC Milan.
Ronaldo amesema kuwa walianza mchezo huo wakijihisi kuwa na uwezo, tulifahamu kuwa tunacheza na timu yenye uzoefu na tulihitaji kuwashambulia, na kama tutafanya hivyo hawataweza kuhimili. Kocha Jose Mourinho, aliwasifu wachezaji wake kwa kusema ninafuraha sana kwa matokeo haya na nina furaha kutokana na jinsi timu ilivyocheza na kuonyesha juhudi. Nafikiri timu hii ilicheza mchezo kamili.
Ajax Amsterdam iliishinda Auxerre kwa mabao 2-1 wakati Sporting Braga walipata points zao za mwanzo katika kinyang'anyiro hiki kwa kuizamisha Partizan Belgrade kwa mabao 2-0 nyumbani Ureno.
Katika mchezo uliochezwa mwanzo Chelsea ilichukua usukani wa kundi F baada ya kuishinda Spartak Moscow kwa mabao 2-0. Nayo Olympique Marseille ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zilina ya Slovakia.