Vifaru vya Syria vyaondoka Homs, waangalizi wawasili | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.12.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vifaru vya Syria vyaondoka Homs, waangalizi wawasili

Vifaru vimeanza kuondoka katika mji wa Homs vilivyokuwa vimeuzingira kwa siku kadhaa, huku waangalizi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wakiwasili kwenye mji huo kutathmini madhara ya operesheni ya kijeshi iliyouwa watu 34.

Ujumbe wa Mawaziri ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Ujumbe wa Mawaziri ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Kiasi ya vifaru 11 vimeonekana asubuhi ya leo vikiondoka katika mtaa wa Baba Amri kwenye viunga vya mji wa Homs. Mmoja wa wanaharakati na mkaazi wa mtaa huo, Mohammed Saleh, amesema mashambulizi makali kutoka mizinga ya vifaru hivyo yalisimama mapema alfajiri, na asubuhi vifaru vikaanza kuondoka.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kutokea nyumbani mwake, upande wa mashariki wa mtaa Baba Amr, Saleh amesema kwamba binafsi ameviona vifaru sita, milango ya saa mbili asubuhi kwa saa za Mashariki ya Kati, vikiondoka.

Kuondoka kwa vifaru kwenye mji wa Homs, ambao tangu Jumapili ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wapatao 4,000, kunasadifiana na wachunguzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuelekea huko, kujionea wenyewe maafa yaliyotokea. Watu 34 waliuawa hapo jana kufuatia operesheni ya kijeshi, dhidi ya kile serikali inachokiita 'uasi wa makundi ya kigaidi yenye silaha.' Hatua ya kupelekwa kwa waangalizi hao, hata hivyo, imecheleweshwa kwa siku kadhaa.

Waandamanaji mjini Homs wakiomba msaada wa Umoja wa Mataifa.

Waandamanaji mjini Homs wakiomba msaada wa Umoja wa Mataifa.

Televisheni ya serikali ya Syria, Dunia, imewaonesha waangalizi hao wakikutana na gavana wa Homs muda mchache uliopita. Mkuu wa ujumbe wa waangalizi hao, Mohammed al-Dabi kutoka Sudan, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hadi sasa serikali inatoa mashirikiano mazuri. Mapema akielezea malengo ya safari yao, mwangalizi kutoka Morocco, Talaa al-Saud al-Atlasy, alisema ujumbe huo unaangalia ikiwa serikali ya Syria imetekeleza makubaliano ya Jumuiya hiyo.

"Tunakwenda kuangalia na kuripoti ikiwa serikali imeondosha watu wenye silaha kutoka mitaani, ikiwa imeweka mazingira mazuri kwa vyombo vya habari kuripoti, na ikiwa imewaachia wafungwa wa kisiasa." Amesema Al-Atlasy.

Kutumwa kwa ujumbe huu ni sehemu ya mpango uliosainiwa na serikali ya Syria hapo Novemba 2, lakini tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo, serikali ya Bashar al-Assad imezidisha maradufu operesheni yake ya kijeshi dhidi ya waandamanaji, ambao nao hawaoneshi dalili ya kusitisha maandamano yao, yanayoendelea kwa mwezi wa tisa sasa.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 5,000 wameshauwa tangu maandamano hayo yaanze mwezi Machi. Mauaji katika mji wa Homs, ambao umekuwa kitovu cha upinzani, yamechochea shinikizo la kimataifa dhidi ya utawala wa Assad, huku upinzani ukiutaka Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuingilia kati, kumaliza kile ulichokiita 'msiba'.

Waandamanaji mjini Homs wakishiriki mazishi ya watu waliouawa na vikosi vya serikali.

Waandamanaji mjini Homs wakishiriki mazishi ya watu waliouawa na vikosi vya serikali.

Hata hivyo, tayari kuna taarifa kwamba serikali ya Syria ndiyo inayoratibu maeneo na safari zote za waangalizi hao wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, jambo ambalo linaweza kuzuia ukweli kubainika.

Katika mji wa Idlib, inasemekana maafisa wa serikali wamebadilisha vibao vya barabarani vinavyoonesha majina ya mitaa kwa lengo la kuwapotosha waangalizi, huku waziri wa mambo ya Nje wa Syria, Walid Muallem, akisema kuwa hatimaye waangalizi hao watathibitisha kuwa makundi ya kigaidi yenye silaha ndiyo yanayofanya mauaji nchini mwake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 27.12.2011
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Maneno muhimu Syria
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13ZhP
 • Tarehe 27.12.2011
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Maneno muhimu Syria
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13ZhP

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com