1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Valerie Amos awasili Goma

8 Agosti 2012

Kamishna wa Masuala ya Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, yuko ziarani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutembelea kambi za wakimbizi wa ndani na baadaye atakwenda Rwanda kujionea hali ya wakimbizi.

https://p.dw.com/p/15ler
Kamishna wa Huduma za Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos.
Kamishna wa Huduma za Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos.Picha: AP

Akiwahutubia na waandishi wa habari baada ya kukutana kwa mazungumzo na Naibu Gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Bi Amos, alisema madhumuni ya ziara yake ni kutathmini mwenyewe hali ya kibinaadamu na kuona namna Umoja wa Mataifa na serikali ya Congo zinaweza kushirikiana kukabiliana na hali ilivyo.

Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa amewasili Goma baada ya kuwa ameshakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali kuu ya Kinshasa. Miongoni mwa vituo vya ziara yake ni kutembelea kambi za wakimbizi wa ndani, zikiwemo za Kanyaruchina iliyo nje kidogo ya mji wa Goma, Rutshuru pamoja na Walikale, ambamo atazungumza na wasimamizi wa kambi hizo kujuwa hali halisi wanayokabiliana nayo.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Fallare Lutahichirwa, amesema wanafurahishwa na hali hii ya mshikamano "katika wakati huu mgumu." Naibu Gavana huyo ameongeza kwamba wanaikaribisha hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa kwani imekuja wakati muafaka.

"Kwetu ni wakati muafaka...atajionea mwenyewe kwa macho yake mawili, hali inayojiri hapa atakapotembelea wakimbizi, atapata picha halisi ya mambo, ambayo itamsaidia kuwatetea wakimbizi ili wapate msaada wa kiutu.” Amesema Lutahichirwa.


Ziara itajumuisha wakimbizi walioko Rwanda

Baada ya kutembelea kambi mbalimbali za wakimbizi katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Bi Amos atazungumza na waandishi wa habari kuwaeleza alichokiona katika ziara yake sio tu mkoani Kivu, bali katika maeneo yote aliyokwenda ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Familia za Kikongo zikikimbia mapigano Kivu ya Kaskazini.
Familia za Kikongo zikikimbia mapigano Kivu ya Kaskazini.Picha: Reuters

Baada ya Goma, Amos ataelekea Rwanda, ambako atakutana pia na wakimbizi wa Kikongo walioko Rwanda. “Nitakwenda kutathmini pia hali ya wakimbizi wa Congo walioko Rwanda, ambao walikimbia kutokana na vita vinavyojiri katika mkoa huu wa Kivu ya kaskazini.” Amesema Amos.


Ziara hii ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinaadamu na Misaada ya Dharura inafanyika wakati hali ikiwa imetulia kwenye uwanja wa mapigano, ambako kumekuwa na vita baina ya waasi wa M23 na jeshi la serikali katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini tangu Aprili 2012.

Waasi wa M23 ni sehemu ya kundi la wapiganaji waz amani wa chama cha uasi CNDP waliokua wanahudumu katika jeshi la serikali na kujiondoa katika jeshi hilo wakilalamikia mishahara na hali duni za maisha. Vita hivyo vimewapelekea raia wapatao 200,000 kuyahama makaazi yao na kukimbilia mwahala mwengine ndani na nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Goma
Mhariri: Mohammed Khelef