1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzinduzi wa bandari ya Lamu

2 Machi 2012

Mradi wa ujenzi wa bandari mpya katika kisiwa cha Lamu nchini Kenya unaanza rasmi baada ya sherehe za kuweka jiwe la msingi hivi leo. (02.03.2012)

https://p.dw.com/p/14D2B
Wakaazi wa Lamu wapinga ujenzi wa Bandari
Wakaazi wa Lamu wapinga ujenzi wa BandariPicha: Reuters

Mradi huu unaokusudiwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 30, ndio mradi mkubwa zaidi kutekelezwa kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini kwa alengo la kuyaunganisha kibiashara mataifa haya.

Lakini kama anavyotuarifu mwandishi wetu aliyeko kisiwani Lamu, mradi huu unakumbwa na pingamizi kubwa kutoka kwa wakaazi wa kisiwa hicho walioandamana kwa amani kwa kile wanachokidai kubaguliwa na serikali ya Kenya katika utekelezaji wake.

Katika muda wa siku nne zilizopita, mji wa Lamu umekuwa ukipokea idadi kubwa ya wageni wa tabaka mbalimbali ambayo haijawahi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni. Rais Mwai Kibaki wa Kenya, hii leo anatarajiwa kuwaongoza viongozi wa nchi na serekali, akiwemo rais wa Sudan ya Kusini Salva Kiir, na waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi katika kuzindua rasmi mradi huu wa ujenzi wa bandari hii mpya kisiwani Lamu.

Bandari ya Mombasa
Bandari ya MombasaPicha: dapd

Bandari hii inayokusudiwa kufungua eneo zima la kaskazini mwa Kenya, hadi nchini Ethiopia na Sudan Kusini ndio itakayokuwa ya pili kwa ukubwa katika kanda hii ya Afrika Mashariki hadi kusini baada ya ya ile ya Durban nchini Afrika Kusini.

Pia mradi huu unaojumuisha ujenzi wa reli, barabara ya kisasa, bomba la mafuta kutoka kisiwani Lamu hadi Sudan Kusini, pamoja na kiwanda cha kusafishia mafua ya petroli, unakusudiwa kupanua biashara baina ya nchi hizi tatu hadi eneo la maziwa makuu.

Wakaazi wa Lamu wapinga

Hata hivyo, wakaazi wa kisiwa cha Lamu tayari wamefika mahakamani kutaka kusimamisha mradi huu, wakidai kuwa serikali ya Kenya imewapuuza katika hoja zao, kwamba huenda mradi huu utakuwa na athari kubwa za kimazingira, mbali na kubaguliwa kwa jamii hiyo katika maswala ya kitaifa ya uchumi na maendeleo.

Wakaazi hao waliandamana baada ya kufanya maombi na kuelezea hoja zao. "Kuanzia ukoloni mpaka kufikia serekali huru za awamu tatu, haijatumilikisha ardhi zetu, bali imewamilikisha wageni kutoka bara, wengi wao wakitoka jimbo la kusini. Mambo ya mazingira, wazee wetu walikuwa wakikata mikoko na kupanda. Leo ukienda kutembea sehemu ya bandari, tayari watu wakata mikoko kupitia misumeno ya umeme. Mnyama aitwae kasa, huenda kizazi kijacho kisimjue...".

Mwenyekiti wa shirika la kiislamu la kutetea haki za binadamu, Khalid Hassan, anasema kuwa "serikali haijaonesha juhudi zozote za kutatua matatizo hayo yanayowakumba wakaazi wa Lamu ambao wamebakia nyuma kimaendeleo tangu Kenya kujipatia uhuru. " Tunaambiwa kuwa watu wa Lamu watapewaa kazi, na hio si kweli. Tunaona hivi sasa tayari vile wameanza, wakaazi wenyewe wa Lamu hawajapewa zile nafasi chache ambazo hivi sasa zinasaidia katika kuanzisha huo mradi".

Serikali yajitetea

Kupitia katibu mkuu wa wizara ya Uchukuzi nchini Kenya Sairas Njiru, ambae alikuwa na wakati mgumu kuutuliza umma, alisema kuwa serikali haina nia yoyote ya kumdhulumu mkaazi asilia wa eneo hili, akiongeza kuwa hoja zote zinzotolewa na wakaazi hao ni za msingi na tayari zinalindwa chini ya katiba mpya ya Kenya. "Ukiongea kwamba mradi utajengwa na watafaidi wengine, ni kana kwamba hatujui kwamba katiba ya siku hizi hairuhusu kuajiriwa kwa mtu yoyote bila kutoa nafasi sawa kwa kila mtu. Pili, ukiangalia sheria iliyopitishwa na bunge wiki jana, imetoa masharti kwamba huwezi kuajiri zaidi ya asilimia sabini kutoka nje ya nchi".

Hali ya usalama imedumishwa katika visiwa vyote vya Lamu, vinavyopakana na nchi jirani ya Somalia, ambako jeshi la Kenya linaendeeza vita dhidi ya wafuasi wa kundi la kigaidi la Alshabab.

Mwandishi: Eric Ponda

Mhariri: Josephat Charo