1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Uvuvi uharibifu kupigwa marufuku

Umoja wa Ulaya unatazamia kuwa na sheria zitakazozingtia tatizo la uvuvi unaopindukia kiasi.Lakini wanachama wa umoja huo hawavui katika bahari za nyumbani,bali hata katika pwani ya Afrika ya Magharibi.

Hadi hivi sasa sera za Umoja wa Ulaya zilizohusika na sekta ya bahari zilitekelezwa na idara mbali mbali za Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kama vile mazingira,uchukuzi,nishati na uvuvi. Lakini yote hayo yanatazamiwa kufanyiwa mabadilisho.

Rais wa Kamisheni ya umoja huo,Jose Manuel Barroso,anaamini kuwa Ulaya inapaswa kutia zaidi maanani maeneo ya bahari,kwani sehemu kubwa ya hatima yake ipo katika utajiri wa baharini. Kuanzia mwezi huu hadi mwaka 2008 au 2009, Kamisheni ya Ulaya itazindua mipango tofauti itakayobadilisha au kuunda sheria mpya za Umoja wa Ulaya kwa azma ya kuchangamsha ukuaji wa kiuchumi na ajira katika sekta ya bahari.

Upande wa uvuvi,kamisheni hiyo inataka kuwazuia wavuvi wa haramia kwa kuongeza urasimu na hata kuwazuia kuingia bandarini na samaki waliovua kinyume na sheria.Uvuvi wa haramia si jambo jipya huku Ulaya au kwengineko.Lakini tatizo hilo limegonga vichwa vya habari kwa sababu akiba ya samaki imepunguka hadi kuwepo haja ya kuruhusu kuvua kipimo fulani tu.

Sheria mpya zitapiga marufuku uvuvi wa uharibifu,ambapo meli hutumia nyavu zinazosomba samaki katika uvungu wa bahari.Vile vile kutakuwepo sheria za kuzuia mtindo wa kutupa samaki wasiohitajiwa.Lakini si meli kubwa za uvuvi kutoka Ulaya peke yake zinazoteketeza raslimali ya baharini.

Kwa mujibu afisa wa shirika la msaada wa maendeleo ya kiufundi la Ujerumani GTZ,bwana Michael Vakily asilimia 80 ya samaki katika pwani ya Senegal huvuliwa na wavuvi wa kienyeji wanaopata msaada wa maendeleo.Vakily amesema:

„Ikiwa watu hawatoruhusiwa tena kuvua,basi kutakuwepo maelfu kadhaa wasio na kazi mjini Dakar na hali hiyo bila shaka itazusha mripuko wa kijamii.“

Lakini tatizo ni kuwa wavuvi hao hufanyia kazi mashirika makubwa yanayojiepusha na gharama za kulipia leseni na hukwepa viwango vya uvuvi kwa kununua samaki kutoka kwa wavuvi wadogo wa kienyeji.

Kwa Wasenegali wengi,uvuvi ni njia pekee ya kuendesha maisha.Hata hivyo,serikali ya Senegal mjini Dakar,imepiga marufuku uvuvi,katika sehemu kadhaa za pwani yake katika juhudi ya kuzuia uvuvi uharibifu kwani hatima yao inategemea raslimali ya bahari.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com