1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yakubali kujiunga na mapambano dhidi ya IS

Admin.WagnerD13 Oktoba 2014

Uturuki imeikubalia Marekani kutumia kambi zake za kijeshi kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la kiislamu- IS huku wapiganaji wa kikurdi wakiendelea kupambana na waasi wa IS

https://p.dw.com/p/1DU82
Picha: AFP/Getty Images/A. Messinis

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria limeripoti wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu wamekabiliwa vilivyo na wapiganaji wa kikurdi ambao wameongeza makali ya mashambulizi yao dhidi ya wanamgambo hao mwishoni mwa juma wakisaidiwa na mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Marekani kuulinda mji wa Kobane.

IS wameongeza idadi ya wapiganaji wake mjini humo na kufyatua makombora takriban 11 katikati ya mji huo lakini wapiganaji wa kikurdi wamefanikiwa kupiga hatua kuyasogelea makao makuu ya mji wa Kobane ambayo yaliangukia mikononi mwa wanamgambo mwishoni mwa juma lililopita.

Marekani ina imani itaitokomeza IS

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Cairo wa wafadhili kusaidia kuijenga upya Gaza,waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ana imani mkakati wa nchi yake kulitokomeza kundi la IS utafanikiwa

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/S. Stapleton

Afisa mkuu wa Kobane Idris Nassan amesema mashambulizi ya angani yanayofanywa na Marekani katika mji wa Kobane yamekuwa msaada mkubwa.

Waziri wa ulinzi wa Kobane Ismet Hassan hata hivyo amesema bado suala la kupata silaha bora kwa wapiganaji wa kikurdi ni changamoto kubwa kwani wanamgambo wa IS wana silaha nzito ambazo walizipora kutoka kwa kambi za kijeshi za Syria na Iraq.

Hata hivyo katika nchi jirani ya Iraq,wapiganaji wa IS wanazidi kuwapa wanajeshi wa taifa hilo kibarua kigumu. Bomu la kutegwa kando ya barabra lilimuua mkuu wa polisi wa jimbo la Anbar na kaskazini mwa Iraq,wanajeshi na wapiganaji wa kisunni walishambuliwa na wanamgambo wa IS.

Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO imekuwa ikisita kujihusisha katika mapigano yanayoendelea nchini Syria na imekuwa ikishinikizwa na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kusadia katika kuukoa mji wa wakurdi wa Kobane.

Uturuki yakubali kushirikiana na Marekani

Katika mazungumzo kupitia njia ya simu na waziri wa ulinzi wa Uturuki Ismet Yilmaz,waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema Uturuki sasa imekubali kushirikiana nayo na ameishukuru kwa kujitolea kwake kuchangia katika juhudi za kukabiliana na kundi la wanamgambo wa dola la kiislamu Syria.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa

Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ametaka kuungwa mkono kijeshi kwa upande wa upinzani nchini Syria wenye msimamo wa wastani ili kuunda kile alichokitaja kikosi cha tatu kitakachokabiliana na utawala wa Syria pamoja na wanamgambo wa IS.

Wakati huo huo, viongozi wa kijeshi wa muungano unaongoozwa na Marekani dhidi ya IS wanatarajiwa kufanya mikutano ya kupanga mikakati leo na kesho mjini Washington. Zaidi ya wakuu 20 wa kijeshi wanatarajiwa kuhudhuria mikutano hiyo ya ngazi ya juu.Miongoni mwa mada za mikutano hiyo ni kutoa mafunzo kwa waasi wenye misimamo ya wastani wa Syria.

Huku hayo yakijiri,waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier hapo jana alifanya mazungumzo na mwenzake wa Saudi Arabia mwana mfalme Saud Al Faisal mjini Jeddah,kuhusu kitisho cha IS. Majeshi ya nchi hizo mbili yanasaidia katika vita dhidi ya wanamgambo hao.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa/ap

Mhariri: Yusuf Saumu