Uturuki itahadhari kuwapiga PKK - Magazeti | Magazetini | DW | 20.10.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uturuki itahadhari kuwapiga PKK - Magazeti

Miongoni mwa mada kubwa za leo (20.10.2011) ni pamoja na kujiingiza kijeshi kwa Uturuki huko Iraq na pia suala zima la mgogoro wa madeni kwenye eneo linalotumia sarafu ya euro, ambapo hadi sasa suluhisho halijapatikana.

Wanajeshi wa Uturuki wakiwa katika jimbo la Simak, lililo mpakani na Iraq.

Wanajeshi wa Uturuki wakiwa katika jimbo la Simak, lililo mpakani na Iraq.

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anasema kwamba mataifa matatu ya Uturuki, Iran na Iraq ni eneo ambalo kundi la Kikurdi la PKK limejikita kwa siku nyingi.

Hata hivyo, operesheni ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya kundi hilo ndani ya Iraq hivi sasa, inapaswa pia kuhakikisha kuwa haiwagusi Wakurdi wa kawaida wa Iraq, maana si kila Mkurdi ni mwanachama wa PKK.

Mhariri huyo anaendelea kusema kuwa, hasira wa Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na za Waturuki, zinafahamika, baada ya kuuawa kwa wanajeshi wake 20 Jumanne iliyopita. Lakini kosa halilipwi kwa kosa.

Suluhisho la kijeshi halikuweza kufanikiwa hapo mwanzo, na halitaweza kufanikiwa hii leo. Wakurdi lazima wapatiwe mamlaka zaidi ya kujiamulia mambo yao. Na huo ni uamuzi mgumu, lakini muhimu sana kisiasa, ambao lazima Erdogan aufikie.

Eneo linalotumia sarafu ya Euro liko kwenye wakati mgumu.

Eneo linalotumia sarafu ya Euro liko kwenye wakati mgumu.

Mgogoro wa madeni kwenye kanda ya euro unaonekana kuwa mada ya kudumu kwenye magazeti ya Ujerumani. Mhariri wa Neue Westfälische Bielefeld anauona kuwa huu ni msiba wa wengi, hauna kilio.

Mhariri huyo anasema kuwa, hata kama Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, anathibitisha kuwa nchi yake nayo itakumba sehemu ya euro bilioni 221 kutoka mfuko maalum wa kuinusuru sarafu ya euro, EFSF, hilo halihakikishi kuwa, Ujerumani nayo siku moja haitajikuta mahala ilipo Ugiriki hivi leo.

Mhariri anasema kuwa, kinacholeta wasiwasi huo ni kuwa, hivi sasa tayari soko la hisa la Frankfurt, liko kwenye wakati mgumu. Benki nazo, hazina uhakika kamili, wa kesho na keshokutwa zitawakuwaje.

Anamalizia mhariri wa Neue Westfälische Bielefeld, kwa kusema kuwa kinachoulizwa hapa sio ukubwa wa tatizo lililopo sasa, bali umbali ambao mgogoro huu utakwenda.

Bendera ya Ujerumani

Bendera ya Ujerumani

Na kwa wale wanaodhani kwamba Ujerumani ni ardhi ya haki, usawa na uadilifu tu, mhariri wa Leipziger Volkszeitung anawakumbusha wafikirie upya.

Mhariri huyo anamnukuu kiongozi wa Jumuiya ya Vijana na kiongozi wa CDU Bungeni, Philipp Mißfelder, akisema: "Kuna ombwe la wazi la haki hapa Ujerumani. Watu wengi kufanya kazi tangu mawiyo hadi machweo, lakini kwa miaka kadhaa hawajawahi kuongezewa mshahara. Ila wakati huo huo, meneja analipwa kile kisichofikirika kwa mtu wa chini."

Hili, anasema mhariri huyo, halivumiliki, ingawa ndio ukweli wenyewe. Ndio ukweli kwamba hadi leo, wengi hawajakishuhudia maishani mwao kile kinachoahidiwa na wanasiasa kuhusiana na haki, usawa na uadilifu kwenye jamii.

Leipziger Volkszeitung linamnukuu tena Mißfelder akimalizia kuwa: "Leo hii Ujerumani inapoonesha mshikamano wake na mataifa ya Ulaya yaliyo kwenye mgogoro wa madeni, inapaswa pia kujiangalia ndani ikoje. Kama tunalipia kuyaokoa mabenki yasifilisike, tunalipaje kumuangalia mfanyakazi asidhalilike."

Vyanzo: Neue Osnabrücker/Neue Westfälische Bielefeld/Leipziger Volkszeitung
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo