Ushawishi wa Uturuki kwa Syria ni mdogo | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ushawishi wa Uturuki kwa Syria ni mdogo

Uturuki haijafanikiwa katika jitahada zake za kumshawishi Rais wa Syria Bashar al-Assad kufanya mageuzi badala ya kutumia mabavu, jambo linalodhihirisha kuwa ushawishi wa Uturuki kwa serikali ya Syria si mkubwa sana.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan

Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan

Kwa miaka kumi iliyopita, Uturuki, iliyo mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO imekuwa ikizipa usogo nchi za Magharibi na kutafuta kujenga ushawishi wake kwenye mataifa mengine, yakiwemo ya Kiarabu.

Lakini kufuatia mapinduzi ya hivi karibuni katika nchi za Kiarabu, picha mpya iliyoibuka, imeonyesha kuwa Uturuki haina ushawishi mkubwa katika nchi hizo, kinyume na matumaini yake.

Katika masuala ya kigeni, Uturuki imefuata sera ya kumaliza matatizo ya zamani na majirani wake, kuimarisha biashara na kuwa dola lenye usemi katika kanda hiyo.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayip Erdogan, anasema wimbi la mapinduzi lilipoanza kupiga nchini Tunisia, alimshauri Rais al-Assad kufanya mageuzi nchini mwake. Alimpeleka mkuu wake wa upelelezi mji mkuu wa Syria, Damascus, kujaribu kumshawishi Assad kufuata njia ya mageuzi, lakini hakufanikiwa.

Miaka miwili iliyopita, Erdogan alipolaani mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, kiongozi huyo aliheshimiwa katika ulimwengu wa Waarabu.

Lakini tangu wimbi la mapinduzi kuanza kusambaa Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati, kiongozi huyo wa Uturuki anatazama kwa tahadhari jinsi viongozi wa Kiarabu wanavyotumia mabavu na kusababisha vifo vya waandamanaji wanaogombea demokrasia.

Kwa mujibu wa Walid Saffour, ambaye ni rais wa Halmashauri ya Haki za Binadamu ya Syria yenye makao yake mjini London, hivi sasa Iran ina ushawishi mkubwa zaidi nchini Syria kuliko Uturuki.

Saffour anasema ikiwa serikali ya Syria itasikiliza lugha ya mantiki, basi itafuata ushauri unaotolewa na Uturuki. Lakini viongozi wenye misimamo mikali katika serikali ya Syria huenda wakahamakishwa ikiwa Erdogan atawashinikiza kuharakisha mageuzi na kuacha kutumia nguvu dhidi ya wananchi wanaoandamana.

Majuma machache yaliyopita, Erdogan alisema kuwa yeye hana hakika iwapo Assad anazuiliwa kufanya mageuzi, ana wasiwasi kwamba mageuzi hayatosaidia au anashindwa kujiamulia.

Wakati huo huo, baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa Uturuki inataka kuendelea na majadiliano pamoja na viongozi kama Muammar Gaddafi wa Libya na Rais Assad wa Syria, badala ya kuungana na wengine kuwalaani viongozi hao wanaohisi kuwa hawatoathirika hivyo kwa kuendelea na sera zao za mabavu.

Kwa upande mwingine, wakosoaji wanasema Erdogan anasita kuelemea upande mmoja kwa sababu ya maslahi ya kibiashara ya Uturuki nchini Libya na Syria.

Mwandishi: Prema Martin/RTRE
Mhariri: Saumu Yussuf

DW inapendekeza

 • Tarehe 13.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11FXN
 • Tarehe 13.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11FXN

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com