Usanifu majengo wenye ubunifu kutoka Afrika
Shule inayoelea badala ya tofali za zege: Miradi mingi mipya ya usanifu majengo barani Afrika haijengwi kwa kutumia chuma na saruji, bali udongo wa mfinyanzi na mbao. Baadhi ya miradi hii inaonyeshwa mjini Munich.
Boti badala ya basi la shule
Watoto katika wilaya ya Makoko laazima wajifunze kuogelea ikiwa wanataka kwenda shuleni. Kwa sababu wilaya hiyo katikati mwa mji mkuu wa Nigeria Lagos imekumbwa na mafuriko tangu mwezi Machi 2013. Shule inayoelea ni mfano wa usanifu majengo wa kiafrika "Afritecture". Usanifu huu unaweka kando dhana za ujenzi wa kimagharibi na kutegemea zaidi mbinu za kienyeji na vifaa kama vile mbao.
Uogeleaji dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Mfano wa shule inayoelea wilayani Makoko ni moja ya vitu vinavyoonyeshwa katika makumbusho ya usanifu majengo mjini Munich. Wilayani Makoko, nyumba hujengwa juu ya mironjo iliyomo ndani ya maji, lakini kutokana na mbadiliko ya tabianchi, zinazama mara kwa mara. Suluhisho la msanifu majengo wa Kinigeria Kunle Adeyemi: Nyumba zijifunze kuelea. Na ya kwanza kufanya hivyo ni shule.
Inaleta maana kwa jamii
Jamii ya watu hutoa mchango muhimu katika miradi ya usanifu majengo ya kiafrika, "Afritecture". Iwe shule au hospitali, jengo hilo linatumiwa na watu wengi. Fokasi moja: Elimu. Mfano wa hii ni kituo cha utamaduni kilichopo katika mji wa Red Location katika jimbo la Port Elizabeth. Kuanzia mwaka 1998 hadi 2012 zimejengwa makumbusho, nyumba ya sanaa na maktaba pembeni mwa vibanda vya wakaazi.
Ushirikiano wa kazi
Mara nyingi watu wanashirikiana katika ujenzi. Shule hii ya kazi za mikono ya Malaa nchini Kenya ilijengwa kwa ushirikiano wa wakaazi na wanafunzi wa Kijerumani. Shule hiyo ilisanifiwa nchini Ujerumani. Lakini kwa miradi mingi inayoonyeshwa mjini Munich, usanifu umefanywa na wasanifu majengo wa kiafrika.
Matundu ya kupitisha hewa badala ya vioyozi
Kwa mfano Francis Keré kutoka Burkina Faso. Pamoja na muongozaji marehemu Christoph Schlingensief, walibuni kijiji cha Opera katika nchi yake. Ujenzi wake ulikamilika mwaka 2013. Keré alitumia udongo wa mfinyanzi kwa kiasi kikubwa. Faida yake: Matundu ya kupitisha hewa ni nafuu sana, rahisi kutengeneza na hakuna haja ya vioyozi. Wakati wa mchana udongo huhifadhi joto na kulitoa wakati wa usiku.
Kamata upepo
Hosptali ya watoto katika mkoa wa Port Sudan inatumia teknolojia kutoka nchini Iran kuviweka vyumba katika hali ya ubaridi: Bādgire, hili linamaanisha kwa Kiswahili, 'kamata upepo'. Jengo hilo hukamata upepo na kuupeleka sehemu ya chini ya jengo kabla ya kuusambaza katika chumba cha wagonjwa.
Nyumba kama vilima
Afritecture- Mara nyingi majengo hujengwa kwa kuzingatia mazingira yao. Kwa kituo hiki cha maonyesho katika mbuga ya Mapungubwe nchini Afrika Kusini, msanifu majengo kutoka Johannesburg Peter Rich alisanifu mabanda kadhaa yenye kuba. Kama vile vilima, mabanda hayo yanapamba madhari yakiwa yamefunikwa kwa mawe kutoka eneo hilo, ambayo yalisambazwa katika mapaa.
Dhidi ya kuta za zege
Miradi 28 kutoka mataifa kama vile Kenya, Nigeria na Burkina Faso inaonyeshwa mjini Munich. Wanajaribu kuwa vinara wa ukuaji kasi wa miji, bila miradi kama hiyo, nchi nyingi za kiafrika zingejenga majumba marefu tu. Miradi hiyo ya ujenzi inalenga ujenzi wa jadi na mahitaji ya wakaazi wa maeneo husika. Kwa namna hiyo usanifu majengo wa kiafrika unatanguliza mbele utaratibu wa ujenzi asilia.