1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yausaidia utawala Syria kupumua

Admin.WagnerD14 Januari 2016

Wakati utawala wa Syria ulikuwa mashakani kufuatia mkururu wa vipigo katika uwanja wa vita katikati mwa mwaka uliyopita, kampeni ya angani ya Urusi imeusaidia kurejesha maeneo yaliyokuwa yanadhibtiwa na waasi.

https://p.dw.com/p/1HdqS
Russland Syrien Luftschläge Kampfflugzeug
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Kots

Pengine mafanikio makubwa zaidi ya utawala wa Assad tangu kuanza kwa mashambulizi ya angani ya Urusi ulikuwa utekaji wiki iliyopita wa mji wa Salma, uliyoko katika mkoa wa pwani wa Latakia, ambao uligeuka ngome ya waasi baada ya kuuteka mwaka 2012.

Sambamba na hilo, jeshi la Syria linapambana kuuchukuwa mji wa Aleppo, kusonga mbele kuelele kusini mwa mkoa wa kati wa Hama na mashariki mwa Homs, na linafanya mashambulizi katika mji muhimu wa Sheikh Miskeen uliyoko katika mkoa wa kusini wa Daraa.

"Bila shaka uingiliaji wa Urusi umekuwa wa thamani isiyomithilika kwa utawala wa Syria, ambao ulikabiliwa na fedheha ya kushindwa vibaya katikati mwa mwaka 2015," anasema Torbjorn Soltvedt, mkuu wa kanda za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kampuni ya uchambuzi wa hatari ya Verisk Maplecroft.

Wanajeshi wa serikali wakifyatua silaha aina ya bomubomu mkoani Latakia, wakisadiwa na mashambulizi y ndege za Urusi.
Wanajeshi wa serikali wakifyatua silaha aina ya bomubomu mkoani Latakia, wakisadiwa na mashambulizi y ndege za Urusi.Picha: picture alliance/AP Photo/A. Kots

Anasema uingiliaji huo umefanikiwa kuwazuwia kusonga mbele waasi wa jeshi huru la Syria FSA, na muungano wa Jeshi la Kiislamu, na kupunguza mbinyo kwa utawala.

Muungano wa jeshi la Kiislamu, ambao unalihusisha kundi la Jabhatu Al- Nusra lenye mafungano na mtandao wa Al-Qaeda, ulikuwa mwiba mchungu hasa kwa utawala wa Assad mwaka uliyopita baada ya kuuteka mkoa wa Idlib.

Kampeni ya Urusi yawaminya waasi

Lakini mashambulizi ya Urusi yalileta shinikizo jipya kwa vikosi vya waasi, ambapo shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uigereza, lilisema Urusi ilifanya mashambulizi 120 dhidi ya mji wa Salma kabla haujatekwa na vikosi vya serikali ya Syria.

Soltvedt anasema kampeni ya angani ya Urusi itaendelea kutoa mchango muhimu katika mgogoro huo, lakini anatahadharisha kwamba kuna ishara ndogo zinazoonyesha kuwa jeshi la Syria linaweza kurejesha nyuma mafanikio yaliyofikiwa na waasi katika mwaka wa 2015 katika kipindi cha muda mfupi.

Mchambuzi mwandamizi kutoka shirika la IHS Janes, Firas Abi Ali, anasema bila ya shaka utawala ndiyo umeshika mpini kwa sasa, na kwamba ubora wa zana zake na msaada wa angani wa Urusi, vinamaanisha kuwa upande wa upinzani wenye zana duni utalaazimika kuachia maeneo.

Swali lakini ni iwapo jeshi la Syria linao uwezo wa kushikilia maeneo linayoyateka. Upungufu wa wanajeshi, na uwezo wa waasi kuifikia mipaka rafiki, vimedhibiti uwezo wa jeshi hilo kufanya hivyo huko nyuma.

Moshi ukitoka katika eneo la makaazi linalodhibtiwa na waasi mkoani Aleppo, kufuatia shambulizi la ndege za Urusi.
Moshi ukitoka katika eneo la makaazi linalodhibtiwa na waasi mkoani Aleppo, kufuatia shambulizi la ndege za Urusi.Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/B. El-Halebi

Mafanikio madogo kijiografia

Wataalamu wanasema mafanikio ya hivi karibuni ya utawala hayajakuwa makubwa kijiografia. Mwanajiografia wa Ufaransa na Syria Fabrice Balanche, alisema kutwaliwa kwa mji wa Salma, pamoja na kuuteka upya uwanja wa ndege wa kijeshi mkoani Aleppo, na ushindi wa ziada kusini mwa Aleppo viliongeza kiasi cha kilomita za mraba 400 za ardhi iliyochukuliwa na jeshi.

Balanche alisema kiukweli jeshi limerejesha morali, lakini pia alibainisha kwamba utawala huo unategemea zaidi msaada wa Urusi na pia wapiganaji wa Kishia.

Anasema lengo la Urusi hasa ni kuisafisha mikoa ya Jabal Turkman na Jabal Akrad ya Latakia, kwa sababu waasi wanaweza kutishia vituo vyake vya kijeshi katika maeneo hayo kwa urahisi.

Anasema kutwaliwa kwa Aleppo ni muhimu kwa sababu Assad anataka kuendelea kuwa rais wa Syria na Syria inamaanisha Aleppo na Damascus. Ikiwa atatawala Damascus tu, basi atakuwa nusu rais.

Vasily Kashin, mtaalamu katika kituo cha uchambuzi wa mikakati na teknolojia chenye makao yake mjini Moscow, anasema Urusi imeweza kwa sehemu kufanikisha malengo yake - ambayo ni kuzuwia kuanguka kwa utawala na kuunda mazingira wezeshi zaidi kwa mazungumzo.

Majeruhi wa kiraia wakisaidiwa katika mji wa Ariha uliopo mkoani Idlib, baada ya shambulizi la ndege za Urusi.
Majeruhi wa kiraia wakisaidiwa katika mji wa Ariha uliopo mkoani Idlib, baada ya shambulizi la ndege za Urusi.Picha: picture-alliance/AP Photo/Ariha Today

Mashaka juu ya uwezo wa jeshi

Katika eneo la kusini wakati huo, kampeni ya utawala kuutwa mji wa Sheikh Miskeen inaweza kufuatiwa na juhudi za kuitwa miji ya mpakani mwa nchi hiyo na Jordan - Daraa na Nasib, iliyotekwa na waasi Oktoba 2013 na April 2015.

Mchambuzi wa siasa kutoka Jordan Labib Qamhoui, anasema Amman ingependelea utawala uvirejeshe mikononi mwake vituo vya mpakani, licha ya kuunga mkono upinzani, ili kupunguza mzigo wa kulinda usalama uliyonao ufalme huo kwenye mpaka wake na mpaka wa Syria.

Iwapo jeshi la Syria linaweza kuvirejesha vivuko hivyo au la, wachambuzi wanasema mafanikio ya jeshi la Syria hayahakikishi kuwa utawala, ambao unadhibiti karibu asilimia 30 tu ya maeneo yanayokaliwa nchini Syria, utapata ushindi katika muda mrefu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.
Mhariri: Saumu Yusuf