1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zaitisha mazungumzo ya amani kuhusu Syria

Isaac Gamba
13 Oktoba 2016

Urusi na Marekani  zimeahidi kuitisha tena mazungumzo ya amani kuhusu Syria  yanayotarajiwa   kufanyika Jumamosi  mjini Lausanne nchini Uswisi yakiwa na  lengo la kutafuta njia ya kusitisha mapigano nchini humo.

https://p.dw.com/p/2RB8k
USA UN-Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/ZUMA Press/A. Lohr-Jones

Syria katika siku za hivi karibuni imekuwa ikiandamwa na mashambulizi mabaya zaidi ndani ya kipindi cha miaka mitano cha mgogoro huo tangu kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ambapo vikosi vya serikali vikisaidiwa na ndege za kivita za urusi vimekuwa vikifanya mashambulizi makali katika mji wa mashariki wa Aleppo unaodhibitiwa na waasi.

Wakati nchi za magharibi zikiishutumu urusi kutokana na kujihusisha na mashambulizi hayo nchini Syria, Urusi na Marekani zimekuwa zikilaumiana kufuatia kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini humo.

Hivi sasa kumekuwa na msukumo mpya wa kufufua mazungumzo hayo kwa lengo la kutumia njia za kidiplomasia katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo ambapo Marekani  ilitangaza hapo jana  kuwa kutakuwa na vikao viwili vya kujadili suala hilo kimoja kikifanyika Jumamosi mjini Lausanne nchini Uswisi na kingine kitafanyika Jumapili mjini London.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wanatarajiwa kuungana na mawaziri wengine wa mambo ya nje  kutoka Uturuki, Saudi Arabia na Qatar ambapo nchi zote hizo zinaunga pande mbili tofauti katika mgogoro huo.

Hadi sasa hakuna nchi iliyothibitisha mwaliko wa Iran katika mazungumzo hayo,nchi  ambayo inahusika kwa kiwango kikubwa katika mgogoro huo na ambayo pia ni mshirika wa karibu wa Rais wa Syria Bashar al- Assad.

Mazungumzo mengine kufanyika mjini London

Schweiz US Premierminister John Kerry und russischer Aussenminister Sergei Lavrow
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Lamarque

Waziri Kerry anatarajiwa pia  kuwa na mazungumzo ya aina hiyo mjini London hapo jumapili ambapo ataungana na mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, ufaransa na Ujerumani.

Umoja wa Mataifa umesema mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria Steffan de Mistura amealikwa kushiriki mazungumzo hayo ingawa msemaji wake alisema hana taarifa kama mjumbe huyo atahudhuria.

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov  katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha CNN hapo jana alisema anatarajia mazungumzo yatakayofanyika mwishoni  mwa wiki nchini Uswisi yanaweza  yakasaidia  kutoa  mwelekeo mpya  kwa kizingatia pia makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa awali  kati ya Marekani na Urusi ambayo  yamesita.

" Tungependelea kuwa na kikao cha watu wachache kitakachojikita katika masuala machache na siyo kuwa na mijadala kama ile ambayo imekuwa ikifanyika katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa" alisema Lavrov.

Hali ilionekana kuanza kuwa tete katika kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa wakati Urusi ilipolazimika kupiga kura ya turufu juu ya azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria linalohusiana na usitishwaji mapigano.

Rais wa Urusi Vladmir Putin aliishambulia ufaransa kwa kuleta pendekezo hilo la kuilazimisha Urusi kupiga kura hiyo ya turufu na kuishutumu nchi hiyo kwa kuleta hoja hiyo  makusudi  ambayo Urusi ingeikataa.

Hayo yanatokea mnamo wakati mashambulizi mapya ya anga yakifanyika hapo jana mjini Aleppo  ambapo kiasi ya watu saba wameuawa na ikiwa ni siku moja tu baada ya Urusi  kushutumiwa kuzidisha mashambulizi yake katika mji huo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri      :Hamidou Oumilkheir