1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Urusi na China zapinga rasimu ya azimio la Marekani

23 Machi 2024

Urusi na China zimetumia kura zao za turufu kuipinga rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani la usitishaji mapigano katika ukanda wa Gaza. Balozi wa Urusi ameikosoa rasimu hiyo aliyoitaja kama ya "kinafiki."

https://p.dw.com/p/4e35N
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwasilisha vipaumbele vyake vya mwaka 2024.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwasilisha vipaumbele vyake vya mwaka 2024.Picha: KENA BETANCUR/AFP/Getty Images

Licha ya kuwepo kwa miito ya kutaka kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza, rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani la usitishaji mapigano ni ishara ya wazi juu ya msimamo wa hivi karibuni wa Washington kuelekea Israel.

Mara sio moja, Marekani imepinga maazimio kadhaa ya kusitisha mapigano huko Gaza katika baraza la usalama la umoja wa mataifa lakini wakati huu imejaribu kupitisha rasimu ya azimio lenye maandishi yanayohimiza "usitishwaji mapigano kama sehemu ya makubaliano ya kuachiliwa huru mateka."

Urusi na China hata hivyo zilitumia kura zao za turufu kuipinga rasimu hiyo. Moscow ilikwenda mbali zaidi na kuiita rasimu hiyo kama "unafiki." China na Urusi pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu yamesema lugha iliyotumika kwenye rasimu hiyo ni dhaifu mno na kamwe hailengi kuiwekea Israel shinikizo lolote.

Soma pia: Blinken: Nafasi ya kusitisha mapigano Gaza inapungua 

Licha ya pingamizi la Urusi na China, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema wanadiplomasia wataendelea na juhudi za kutafuta mwafaka juu ya maandishi sahihi yanayokubalika na kila upande kwenye rasimu hiyo ya azimio.

Kando na Urusi na China, Algeria pia imepiga kura ya kupinga rasimu hiyo ya azimio japo nchi hiyo sio mwanachama wa kudumu wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakati Guyana ikijizuia kupiga kura na nchi 11 zilizosalia zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo lililopendekezwa na Marekani.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vasily Nebenzia amesema kwa jinsi maandishi yalivyo kwenye rasimu hiyo, itafungua mlango kwa Israel kuendelea kuvunja sheria bila ya kujali.

Marekani yazishtumu China na Urusi kwa kutumia nguzu zao za kura ya turufu

Waandamanaji nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili juu ya mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas.
Waandamanaji nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili juu ya mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas.Picha: David Dee Delgado/REUTERS

Mwanadiplomasia wa Marekani Antony Blinken amezishtumu China na Urusi kwa kutumia nguzu zao za kura ya turufu kwa maslahi yao binafsi huku kundi la Hamas likikaribisha uamuzi uliochukuliwa na Beijing na Moscow.

Hatua ya Marekani, ambayo ni mshirika mkuu wa Israel, ya kuwasilisha rasimu ya azimio la usitishaji mapigano imetolewa wakati kukiwepo mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

Soma pia:  Israel yadai kuwashikilia wanamgambo 500 wa Kipalestina

Marekani imeweka wazi kuwa inatarajia Israel kupunguza makali ya mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza ambapo wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema zaidi ya watu 30,000 - wengi wao wanawake na watoto - wameuawa tangu mapigano yalipoanza mnamo Oktoba 7.

Marekani imeongeza kuwa, haitaunga mkono shambulio la Israel kwenye mji wa Rafah pasi na kuwepo mpango madhubuti wa kuwalinda wakaazi katika mji huo, na imeihimiza Israel kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia Gaza.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wake wataendelea na mashambulizi ya ardhini kwenye mji wa Rafah bila kujali uungwaji mkono wa mshirika wake mkuu, Marekani.

Netanyahu amemueleza Blinken kuwa, hakuna njia nyengine ya kuishinda Hamas bila ya wanajeshi wa Israel kuingia mjini Rafah.

Blinken, akiwa mjini Tel Aviv kwa mazungumzo, ameeleza kuwa oparesheni inayopangwa kufanywa na jeshi la Israel mjini Rafah sio suluhu.

Soma pia: Hamas yaahidi kuendelea na mazungumzo hadi makubaliano 

Zaidi ya nusu ya Wapalestina milioni 2.3 wametafuta hifadhi katika mji huo wa kusini ambako Israel inasema viongozi wa Hamas wamejificha.

Maafisa wakuu wa Israel na Marekani wanatarajiwa kukutana mjini Washington wiki ijayo, ambapo Marekani itapendekeza njia mbadala kwa Israel za kuwawinda wapiganaji wa Hamas bila ya shambulio kamili mjini Rafah.