1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urafiki wa mashaka wa Emmanuel Macron na Donald Trump

Zainab Aziz
25 Aprili 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alifanya ziara ya kwanza ya kiserikali nchini Marekani tangu rais Donald Trump aingie madarakani, Je! amepata mafanikio ya kuanzisha uhusiano wa karibu na mwenzake wa Marekani?

https://p.dw.com/p/2wc8f
USA Washington - Donald Trump trifft Emmanuel Macron
Picha: Reuters/J. Ernst

Julianne Smith mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa taifa wa aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani Joe Biden amesema binafsi hadhanii kama Macron amefaulu kuuanzisha uhusiano wa karibu baina yake na Donald Trump.

Naye mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa masuala ya Ujerumani na Ulaya katika Chuo Kikuu cha Georgetown Jeffrey Anderson, amesema ziara ya kwanza ya kiserikali nchini Marekani ya rais Macron ikilinganishwa na ziara fupi ya wiki ijayo katika jiji la Washington itakayofanywa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ni mfano wa kisiasa unaoonyesha kuwa Macron ndiye kiongozi au dereva wa bara la Ulaya na hasa kwa mtazamo wa Marekani.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/K. Lamarque

Waangalizi wa Trans Atlantic wamesema kupanda kwa haraka kwa umaarufu wa Macron kumetokana na kutoweka kwa muda mrefu kansela Merkel kwenye jukwaa la kimataifa kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi wa Ujerumani ambayo yalisababisha wakati mgumu katika kuunda serikali, hali iliyochangia pakubwa kushuka umaarufu wake hata ndani ya nchi.

Ni mabadiliko ya kushangaza katika matukio ambapo kiongozi huyo mwanamke ambaye si chini ya mwaka mmoja uliopita alitukuzwa kwa kuitwa kiongozi wa ulimwengu wa Magharibi na sasa hivi ni wakati ambapo umaarufu wa Macron umepanda kwa kasi huku umaarufu wa kansela Merkel ukionekana kupungua.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/S. Gallup

Waangalizi hao wamesema Merkel kama kiongozi na Ujerumani kama nchi kwa muda mrefu imekuwa  ni mpokeaji kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na masuala kama vile ya uhamiaji, matumizi ya ulinzi na biashara za ziada baina ya Ujerumani na Marekani. Waangalizi hao wamezingatia ukweli kwamba uhusiano binafsi baina ya Merkel na Trump binafsi ni mgumu kuliko wa Macron na Trump na wamekumbusha hasa sehemu iliyojadiliwa sana ya kupeana mkono viongozi hao wakati wa ziara ya kwanza ya kansela Merkel katika ikulu ya Marekani.

Naibu mkurugenzi wa mpango wa Ulaya wa kituo cha mkakati na masuala ya kimataifa, Jeff Rathke, amesema suala la muhimu ni iwapo Macron atafaulu kutenganisha uhusiano wake wa kibinafsi na Trump na maslahi ya Ufaransa. Swali kubwa ni iwapo uhusiano huo wa kibinafsi ni wa kweli, Rathke ametoa amesema Macron amefanya vizuri kuendeleza uhusiano wa kibinafsi na Rais Trump lakini haijulikani kama ameshapata matokeo ya uhusiano huo wa kibinafsi na kuuliza je utakuwa tofauti na ule anaoutaka kansela wa Ujerumani Angela Merkel?

Marais wa Marekani Donald Trump na wa Ufaransa Emmanuel Macron
Marais wa Marekani Donald Trump na wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/J. Bourg

Naibu mkurugenzi huyo amesema matamshi ya Trump baada ya kukutana na Macron siku ya Jumanne, hayaonyeshi kama kuna tamaa ya kupatikana mafanikio hasa katika masuala manne muhimu ambayo ni maamuzi ya Trump juu ya makubaliano ya nyuklia ya Iran, kuongezwa muda wa wanajeshi wa Marekani huko nchini Syria, mkataba juu ya mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris na ushuru wa Marekani dhidi ya Ulaya. Juu ya yote hayo Trump ameonyesha wazi kwamba hayuko tayari kulegeza msimamo wake.

Mwandishi:Zainab Aziz/Knigge Michael/ LINK: http://www.dw.com/a-43516787

Mhariri:Josephat Charo