1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Syria wataka duru ya pili ya mazungumzo iharakishwe

Mjahida21 Machi 2016

Upinzani nchini Syria umesema unapinga hatua yoyote ya serikali ya kuchelewesha duru nyengine ya mazungumzo ya amani hadi baada ya uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 mwezi Aprili,

https://p.dw.com/p/1IGsl
Genf Syrien Konferenz HNC Vertreter Opposition Mistura
Baadhi ya viongozi wa upinzani mjini GenevaPicha: Reuters/D. Balibouse

Upinzani umeiomba Urusi kumuhimiza mshirika wake Syria kuingia katika mazungumzo ya dhati ya kutafuta suluhusu la kisiasa katika mgogoro wa nchi hiyo uliyoingia mwaka wake wa tano hivi karibuni.

"Tunajua kuwa utawala wa Syria umetaka kucheleweshwa mazungumzo hayo kwa wiki mbili ili kufanyike duru nyengine ya mazungmzo. Serikali hiyo inajaribu kukwepa jukumu lake kwa kuyachelewesha majadiliano hayo," alisema Yahya Qadamani, Naibu mratibu katika kamati kuu ya upinzani HNC, alipokuwa anazungumza na waandishi habari mjini Geneva.

Yahya Qadamani amesema ni lazima duru nyengine ya mazungumzo ifanyike kwa wakati, huku akisisitiza kuwa serikali ya Syria haina haki ya kuchelewesha mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 4 Aprili.

Schweiz Syrien-Friedensgespräche in Genf
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria Staffan de MisturaPicha: Reuters/R. Sprich

Kwa upande wake msemaji wa kamati hiyo ya upinzani HNC Salim Al-Muslat, amewaambia waandishi habari kuwa hawatakubali ucheleweshwaji wa mazungumzo ili uchaguzi waliyouita haramu kufanyika.

Ameongeza kuwa kamati hiyo bado haijafahamishwa na de Mistura kuhusu ucheleweshwaji wa duru ya pili ya mazungumzo lakini akasema atalizungumzia suala hilo katika mazungumzo yanayoendelea siku ya Jumatatu 21.03.2016

Mazungumzo yanatarajiwa kusimamishwa kwa muda na kuanza tena mwezi Aprili

Rais wa Syria Bashar al-Assad aliitisha uchaguzi huo mwezi uliyopita, akiwa na ujasiri baada ya kuonyesha ushindi katika uwanja wa mapambano katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo. Uchaguzi unafanyika kila baada ya miaka minne na wa mwisho ulifanyika mwaka wa 2012.

Syrien Gefecht in Aleppo
Athari ya mabomu mjini Allepo SyriaPicha: picture-alliance/dpa/Maysun

Pande mbili zinazohasimiana katika mgogoro huo zimekuwa zikifanya mazungumzo tofauti wiki iliyopita mjini Geneva na Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria Staffan de Mistura, aliyesema anapanga kuyasimamisha kwa muda mazungumzo hayo siku ya Alhamisi hadi mwezi Aprili.

Wajumbe wa upande wa serikali ya Syria wanakabiliwa na shinikizo la kujadili hatma ya rais Bashar al Assad jambo linalopendekezwa na upinzani.

Huku hayo yakiarifiwa Urusi imeishutumu Marekani kwa kusitisha utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria yaliyoanza kutekelezwa mwezi uliyopita. Urui imeonya kuwa hatua hiyo huenda ikachangia ukiukwaji wa makubaliano hayo. Luteni jenerali Sergei Rudskoy amesema katika taarifa yake kwamba Marekani haijaonyesha kama iko tayari kujadili makubaliano na Urusi.

Mwandishi: Amina Abubakar Reuters/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu