Upinzani nchini Pakistan: Uchaguzi utakuwa kama ″mzaha″ | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Upinzani nchini Pakistan: Uchaguzi utakuwa kama "mzaha"

Baada ya rais Pervez Musharraf wa Pakistan kutangaza kwamba uchaguzi utafanyika, mwanzoni wa mwezi wa Januari, mwaka ujao, vyama vya upinzani vilimlaani rais huyu na kusema uchaguzi huo hautakuwa wa haki kabla ya sheria ya hali ya hatari haijaondoshwa.

Waandishi wa habari wa Pakistan waliandamana dhidi ya uthibiti wa vyombo vya habari

Waandishi wa habari wa Pakistan waliandamana dhidi ya uthibiti wa vyombo vya habari

Wiki moja baada ya kutangaza sheria ya hali ya hatari nchini Pakistan, rais Musharraf jana aliarifu kuwa uchaguzi wa bunge la taifa na mabunge manne ya mikoa utafanyika kabla ya tarehe tisa Januari. Tarehe kamili lakini ni juu ya tume ya uchaguzi kuamua. Kwa kuchukua hatua hiyo, Musharraf alilikubali shinikizo la ndani na nje, lakini kwa kiasi fulani tu. Bado hajasema hali ya hatari itaisha lini.

Ndiyo sababu vyama vya upinzani vimetoa mwito kwa raisi huyo kuondoa hali ya hatari la sivyo uchaguzi huo ujao utakuwa kama mzaha tu, kama alivyosema waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif: “Majaji walikamatwa na serikali, hakimu mkuu anazuiliwa nyumbani, majaji walifukuzwa mahakamani na kuna majaji wapya waliochaguliwa na serikali. Pia tume ya uchaguzi haiko huru – kwa hivyo ni aina gani ya uchaguzi Bw. Musharraf anataka kuufanya? Mimi nadhani utakuwa mzaha tu!”

Vyama kadhaa vinafikiria kususia uchaguzi huo. Lakini rais Musharraf alitetea uamuzi wake wa kutangaza hali ya hatari. Kama sababu, alitaja mapigano kati ya jeshi la wanamgambo wa Taliban pamoja na mashambulio ya kigaidi nchini kote: “Kwa kuzingatia hali ilivyoharibika, mazingira ya kigaidi, mashambulio ya kigaidi na hali ngumu ya usalama kwenye mipaka ya Afghanistan, basi ni hali hiyo ya hatari ambayo itaweza kuongeza juhudi na kuthibiti magaidi. Tutakuwa na uchaguzi huru, wazi na wa haki.”

Musharraf vile vile aliahidi kujiuzulu jeshini na kuapishwa kama rais pale Mahakama Kuu itakapoidhinisha hatua iliyomchagua kuendelea na wadhifa huo. Kulingana na ripoti kwenye gazeti moja la Pakistan leo hii, mahakama kuu ya nchi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikiliza kesi dhidi ya ushindi wa rais Musharraf akiwa bado mkuu wa jeshi hapo mwaka 2002.

Rais Musharraf alitangaza hali ya hatari tarehe tatu mwezi huu na kuwafukuza kazini majaji wakuu pamoja na kuwakamata mawakili, wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu. Rais alitetea hatua hiyo kwa kusema majaji hao walizuia vita dhidi ya wanamgambo wa Taliban na kujiingiza katika mambo ya kisiasa. Wanadiplomasia kadhaa lakini wanasema Musharraf alilenga hasa kuizuia makahama kuu kuamua kwamba ushindi wake kwenye uchaguzi kutokuwa halali.

Kiongozi wa upinzani, Bi Benazir Bhutto ambaye pia anadai hali ya hatari iondolewe na uchaguzi kufanyika haraka, alipongeza taarifa ya Musharraf juu ya uchaguzi lakini wakati huo huo alitaka hatua nyingine zichukuliwe kwa sababu uchaguzi huru na wa haki hautawezekana chini ya hali ya hatari. Benazir Bhutto pia aliarifu kwamba ataendelea na kampeni yake ya upinzani. Bibi Bhutto aliwasili mjini Lahore ambapo kesho anataka kufanya maandamano makubwa ya masafa ya kilomita 275 hivi hadi mji wa Islamabad ambapo analenga kuongeza shinikizo dhidi ya rais Musharraf. Bibi Bhutto yuko chini ya ulinzi mkali wa polisi kutokana na tishio la mashambulizi.

Leo hii, maafisa wa serikali na polisi wanatarajiwa kuamua juu ya amri ya kupiga marufuku maandamano haya. Waziri wa sheria wa mkoa wa Punjab alisema maadamano hayaruhusiwi katika hali ya hatari. Chama cha “Pakistan People's Party” cha Benazir Bhutto kilitishia matumizi ya nguvu ikiwa maandamano yatazuiliwa.

 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH74
 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH74

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com