1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uongozi mpya wa CDU Magazetini

Oumilkheir Hamidou
10 Desemba 2018

Uongozi mpya wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union-CDU, hali ya chama cha Social Democratic SPD na maandamano ya vizibao vya manjano nchini Ufaransa ni miongoni mwa mada magazetini hii leo.

https://p.dw.com/p/39nBL
Deutschland Annegret Kramp-Karrenbauer und Paul Ziemiak
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Tunaanza na mageuzi ya uongozi katika chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union-CDU. Chama hicho kimejipatia mwenyekiti mpya, Annegreth Kramp-Karrenbauer- mashuhuri  kwa jina AKK . Nafasi yake kama katibu mkuu amekabidhiwa Paul Ziemiak, mwenye umri wa miaka 33. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung " linatathmini mabadiliko ya uongozi ndani ya chama cha CDU na kuandika: "Werevu wa kisiasa anaudhibiti kikamilifu katibu mkuu mpya Paul Ziemiak. Mtu aliyejiunga na tawi la vijana la CDU akiwa na miaka 14 , na tangu alipokua na umri wa miaka 29 , kufanikiwa kuliongoza tawi hilo na wanachama wake laki moja na elfu tano tena bila ya lawama, ni stadi tu.

Mbinu na werevu ni sifa anazostahiki kuwa nazo katibu mkuu, sawa na kuzingatia mahitaji ya vijana. Lakini wana CDU wenye kujiamini wana kiu cha uwazi na ahadi thabiti. Yalikuwa dhaifu matokeo ya zoezi lililomtwika Ziemiak jukumu hilo kubwa. Anakabiliwa na kishindo cha kukiunganisha chama na kukipunguzia machungu ya kushindwa Friedrich Merz. Maarifa aliyojipatia katika uongozi wa tawi la vijana yatamsaidia. Seuze ameshadhihirisha anaweza , alipoyanusuru makundi ya vijana wa CDU na CSU yasigawike kutokana na mzozo wa wakimbizi."

SPD wana mbinu gani?

Katika wakati ambapo CDU wanajipa matumaini kwa kujipatia uongozi mpya, wenzao wa SPD bado wanatanga. Gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaandika: "Hali imezidi kuwa mbaya katika chama cha SPD kutokana na kuchaguliwa Annegret-Kramp-Karrenbauer kukiongoza chama cha CDU. Dhidi ya Merz wana SPD wangekuwa na msimamo bayana na mkali zaidi. Na pengine ushindi wa Merz ungesababisha uchaguzi kuitishwa kabla ya wakati, hatua ambayo SPD hawako tayari kuiunga mkono ingawa ndio hatua pekee itakayowapatia fursa ya kujifanyia marekebisho. SPD, sawa na mwenyekiti wake Andrea Nahles wamebakia kivuli tu."

Vizibao vya manjano waitia kishindo serikali ya Ufaransa

Waandamanaji wanaojiita " vizibao vya manjano" wanaendelea kufanya fujo katika miji tofauti mikubwa ya Ufaransa. Madai yao yanazidi kuongezeka : baada ya kulalamika dhidi ya nyongeza ya kodi ya mafuta ya petroli, hivi sasa wanalalamika dhidi ya mishahara mikubwa mikubwa ya wabunge na kadhalika. Gazeti la Weser-Kurier" linajiuliza rais Emmanuel Macron atafanya nini? "Litakuwa kosa kubwa kama rais Macron ataachana na mpango wake wa mageuzi baada ya  kutangaza azma ya kuufanyia marekebisho kwanza mfomu wa ajira na malipo ya uzeeni. Ili aweze kuidhibiti hali ya mambo atalazimika pengine kubadilisha mbinu . Ni muhimu kwasababu ya kurejesha imani na kufafanua vyema zaidi sera yake. Kazi kubwa kabisa inamsubiri rais Macron.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu