1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Watoto walishambuliwa mno 2017

Caro Robi
28 Desemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, limesema mwaka 2017 ulikuwa miongoni mwa mibaya zaidi kwa watoto wanaoishi katika maeneo ya vita na mizozo duniani.

https://p.dw.com/p/2q1pF
Angola flüchtchtlings Kinder aus Kongo
Picha: UNICEF/N. Wieland

Ripoti ya shirika hilo la UNICEF imesema pande zinazozana katika vita duniani zilikiuka wazi wazi sheria za kimataifa linapokuja suala la kuwalinda watozo. Mkurugenzi wa UNICEF kuhusu mipango ya dharura Manuel Fontaine amesema watoto walilengwa na kuwekwa katika hatari ya mashambulizi wakiwa nyumbani, shuleni na wakicheza.

Fontaine ameongeza kusema ulimwengu haupaswi kuyafumbia macho mashambulizi haya akisisitiza maovu dhidi ya watoto hayapaswi kuwa matukio ya kawaida katika ulimwengu wa sasa.

Maovu dhidi ya Watoto ni makubwa

Watoto katika mataifa yanayoshuhudia vita wamekuwa waathiriwa wakubwa wakiuawa, kulemazwa, kusajiliwa kwa lazima kuwa wapiganaji, kuolewa kwa lazima, kutekwa nyara, kutumikishwa na kubakwa.

Südsudan Kindsoldaten
Watoto wapiganaji wa Sudan KusiniPicha: picture-alliance/dpa/AA/S. Bol

Wengi wa watoto hao wanaathirika katika mataifa ya Syria, Yemen, Nigeria, Sudan Kusini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Myanmar. Mamilioni ya watoto wengine wanakumbwa na utapia mlo, magonjwa, msongo wa mawazo na kukosa mahitaji ya kimsingi kama chakula, maji, na huduma za afya.

Ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia watoto limetoa takwimu kuhusu jimbo la Kasai katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako ghasia zimesababisha takriban watoto 850,000 kuyahama makazi yao na wengine 350,000 kukumbwa na utapia mlo mbaya. Shule 400 nchini Congo zilishambuliwa kimakusudi.

Nchini Nigeria na Cameroon, waasi wa kundi la Boko Haram waliwatumia kiasi ya watoto 135 kama washambuliaji wa kujitoa muhanga kwa mabomu, hiyo ikiwa mara tano ya idadi ya watoto waliotumika na waasi hao mwaka jana.

Wengi wanakumbwa na utapia mlo

Sudan Kusini, zaidi ya watoto 19,000 wamesajiliwa kwa lazima kuwa wapiganaji kuanzia mapigano yalipozuka nchini humo mwaka 2013.

Jemen Kinder Hunger
Mtoto aliye na utapia mlo mbaya YemenPicha: Reuters/K. Abdullah

Nchini Yemen, vita vilivyozuka mwezi Machi mwaka 2015 vimesababisha watozo 5,000 kupoteza maisha yao au kujeruhiwa, huku idadi kamili ikihofiwa kuwa hata juu ya hiyo. Uhaba mkubwa wa chakula nchini humo umesababisha takriban watoto milioni mbili kukumbwa na utapia mlo mbaya.

Nchini Iraq na Syria, kiasi ya watoto 700 wameuawa mwaka huu na UNICEF imeripoti kuwa katika baadhi ya visa watoto nchini humo walitumika kama ngao vitani. Zaidi ya watoto milioni 11 wanahitaji kwa dharura misaada ya kibinadamu.

Ripoti hiyo ya UNICEF inalenga kuufanya ulimwengu kuangazia masaibu wanayopitia watoto walioko katika maeneo ya mizozo duniani na Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuwalinda watoto.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/http://www.dw.com/en/unicef-2017-a-nightmare-year-for-children-caught-in-war-zones/a-41951890

Mhariri: Iddi Ssessanga