1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR yatimiza miaka 60:Wakimbizi wanahangaika

Thelma Mwadzaya14 Desemba 2010

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi linaadhimisha miaka 60 tangu kuzinduliwa rasmi.

https://p.dw.com/p/QXyu
Antonio Guterres,Mkurugenzi wa UNHCRPicha: picture-alliance/ dpa

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati ambapo bado suala  la wakimbizi linautatiza ulimwengu mzima pamoja na kuwa na watu wasiokuwa na uraia.Moja ya mataifa yanayokabiliwa na vita na ghasia ni Somalia iliyo jirani ya Kenya na wakimbizi wanaotokea huko huikimbilia.Siku hii inaadhimishwa kote ulimwenguni kukiwa na changamoto nyingi zinazowakabili wakimbizi na wahudumu.

Vyanzo vipya

Akizungumza katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi,UNHCR,Mkurugenzi mkuu Antonio Guterres aliitolea wito jamii ya kimataifa kuziimarisha juhudi zake na mchango ili kupambana na tatizo la wakimbizi.Bwana Guterres alitahadharisha kuwa kuna vyanzo vipya vinavyosababisha watu kuyakimbia mataifa yao.Kiongozi huyo alilielezea pia tatizo la Somalia ambako bado vita vinaendelea na kuwafanya wengi kutorokea nchi jirani ya Kenya.Shirika la UNHCR lina kitengo maalum nchini Kenya kinachowahudumia wakimbizi wa Somalia.Roberta Russo ni msimamizi wa kitengo hicho na anaeleza kuwa''Wengi wao wanaishi katika kambi zilizoko kaskazini mwa Kenya na hali kwa kweli ni mbaya.Kuna uhaba wa maji safi ya matumizi na kambi hizo zina uwezo wa kuwahudumia kiasi ya thuluthi moja tu ya wakimbizi wote wanaohifadhiwa hapo.   

Somalia Mogadischu Flüchtlinge Flash-Galerie
Familia na virago vyao wakizikimbia ghasia za Mogadishu:Watu milioni 1.5 wameachwa bila makazi SomaliaPicha: AP

Kambi za Kenya

Kiasi ya wakimbizi milioni 1.5 wameachwa bila makazi Somalia kwenyewe na laki tatu wengine wamekimbilia nchi jirani ya Kenya na wanahifadhiwa katika kambi za Dadaad na Kakuma.Hivi karibuni taarifa ziliezeza kuwa baadhi ya wakimbizi wa Somalia walioko Kenya wanalazimishwa kurejea walikotokea.Roberta Russo wa kitengo cha Somalia katika shirika la UNHCR anafafanua kuwa'UNHCR imeitolea jamii ya kimataifa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia wanaovikimbia vita.Inaeleweka kuwa serikali ya Kenya inajitahidi kuwa chonjo zaidi kwasababu za kiusalama ukizingatia kitisho cha ugaidi.Hata hivyo bado tunawaomba waendelea kuwaruhusu wakimbizi waingie.' 

Somalia Demosntration in Mogadischu Flash-Galerie
Maandamano ya kuzipinga ghasia:Al Shabaab na makundi mengine wanaivuruga SomaliaPicha: AP

Ili kujaribu kupambana na hali hiyo,Umoja wa Mataifa umetolea wito jamii ya kimataifa kuchangia kiasi ya dola milioni 530 zitakazotumika kuifadhili misaada ya wakimbizi wa Somalia.Zaidi ya kiasi ya wakimbizi laki nne wa Somalia wamelikimbilia eneo la Afgooye lililoko karibu na mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu.Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa idadi hiyo ni kubwa zaidi ulimwenguni ya watu walioachwa bila makazi nchini mwao. 

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-UNHCR website/DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu Ramadhan