1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umwagaji wa damu waendelea nchini Irak

P.Martin6 Agosti 2007

Hii leo mashambulizi mawili nchini Iraq yameua watu 36. Katika mji wa Tal Afar ulio kaskazini mwa nchi, Wairaki 27 waliuawa na wengine 9 nje ya mji mkuu Baghdad.

https://p.dw.com/p/CHA1
Wanajeshi wa Kimarekani kwenye kituo cha ukaguzi ukingoni mwa mji mkuu Baghdad.
Wanajeshi wa Kimarekani kwenye kituo cha ukaguzi ukingoni mwa mji mkuu Baghdad.Picha: AP

Mshambulizi aliejitolea maisha muhanga amewaua Wairaki 27 baada ya kujiripua katika lori lililojazwa miripuko katika kijiji cha Al-Quba ambako Washia wengi huishi na kipo kama kilomita 20 kaskazini ya mji wa Tal Afar.Wengine 50 pia walijeruhiwa katika shambulio hilo,8 wakiwa mahututi.

Wanamgambo nchini Irak wamezidi kufanya mashambulizi yao vijijini na katika maeneo ya mashambani,wakati wanajeshi wa Kimarekani na wa Kiiraki wakiendelea na operesheni iliyoanzishwa miezi mitano iliyopita,kuimarisha usalama katika mji mkuu Baghdad na miji mingine yenye machafuko.

Juu ya hivyo hii leo,watu 9 waliuawa kusini mwa Baghdad,baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripuka kwenye kituo cha basi.Vipande vya bomu vilitawanyika eneo hilo,ambako Wairaki wengi walikuwa wakingojea mabasi kando ya barabara wakiwa njiani kwenda kazini.

Mashambulizi ya leo yametokea huku maafisa wa Kiirani na Kimarekani wakikutana mjini Baghdad katika juhudi za kupunguza machafuko ya waasi nchini Irak.Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Kimarekani aliezungumza kwa sharti kuwa asitajwe kwa jina,mkutano huo umefunguliwa kwenye ofisi ya Waziri Mkuu wa Irak,Nuri al-Maliki katika eneo linalolindwa vikali na ambako kuna ofisi za serikali na ubalozi wa Marekani.Wakati huo huo, mwanadiplomasia mmoja wa Marekani amesema,mkutano huo utashughulikia suala la usalama peke yake.

Kwa upande mwingine shirika rasmi la habari la Iran,ISNA limemnukulu balozi wa Iran nchini Irak, Hossein Kazemi Qomi akisema,majadiliano ya juma hili kati ya Iran na Marekani yatahusika na muundo na dhamana za kamati ya usalama ya pande tatu.

Wajumbe wa Iran na Marekani katika mazungumzo yaliofanywa Julai 24 chini ya uongozi wa Kazemi Qomi na balozi wa Marekani nchini Irak,Ryan Crocker walishindwa kuafikiana juu ya njia za kurejesha usalama nchini Irak.Lakini pande hizo mbili hasimu zilikubali kuunda kamati ya usalama ya pande tatu kwa azma ya kuzuia harakati za wanamgambo pamoja na kupiga vita kundi la Al-Qaeda na kulinda mipaka.Lakini suala la wanamgambo wa Kishia halikutajwa.

Majeshi ya Kimarekani nchini Irak mara kwa mara huyatuhumu makundi yenye uhusiano na Iran kuwa hutoa mafunzo kwa wanamgambo nchini Irak na huwapatia pia miripuko inayoweza kupenyeza mabamba ya vyuma katika magari ya kijeshi ya Marekani.Iran lakini inakanusha mashtaka ya kutoa misaada kwa makundi ya waasi nchini Irak.