Umoja wa Ulaya wasema uchaguzi DRC ulikuwa na dosari nyingi | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 14.12.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Umoja wa Ulaya wasema uchaguzi DRC ulikuwa na dosari nyingi

Kikundi cha wachunguzi wa Umoja wa Ulaya kimeongeza sauti yake kwenye shutuma zinazoongezeka kukosoa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais Joseph Kabila aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi DRC

Rais Joseph Kabila aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi DRC

Tangazo lililotolewa na kikundi hicho lilisema uchaguzi huo ulikosa uwazi katika utaratibu mzima wa kukusanya na kuhesabu kura. Ijumaa iliyopita Rais wa sasa Joseph Kabila alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 49.

Kikundi hicho kiliungana na kituo cha Carter kutoka Marekani, kuelezea wasi wasi juu ya utaratibu uliotumiwa kuhesabu kura, ambao umeshutumiwa kupoteza kura nyingi. Wachunguzi hao walisema kulikuwa na hitilafu katika kukusanya kura kutoka vituo vya uchaguzi, na katika kuorodhesha na kuchapisha matokeo kutoka vituo hivyo.

Zoezi la kukusanya kura limeripotiwa kuwa na hitilafu chungu nzima

Zoezi la kukusanya kura limeripotiwa kuwa na hitilafu chungu nzima

Umoja wa Ulaya ambao ulikuwa na wachunguzi 147 katika maeneo mbali mbali ya nchi, ulisema zoezi la kukusanya kura lilifanywa bila mpangilio, na wakala wa vyama walikatazwa kuingia kwenye vyumba lilimofanyika zoezi hilo. Kwa mujibu wa wachunguzi hao, kuna hata vituo vya uchaguzi ambavyo havikuchapisha kabisa matokeo ya mwisho.

Walisema kuwa baadhi ya matokeo waliyoshuhudia yakirikodiwa usiku baada ya siku ya kupiga kura katika baadhi ya vituo, hayafanani na yale yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hapo baadaye.

Wachunguzi wa umoja wa Ulaya walisema katika tangazo lao kwamba tume ya uchaguzi haikuweza kufafanua ilipokwenda asilimia 7.6 ya kura zilizopigwa nchini kote, ambayo ni sawa na kura milioni moja na laki sita. Kati ya vituo 4,875 ambavyo kura zake hazikuorodheshwa, 2,020 ni kutoka mji mkuu Kinshasa, ambao ni ngome ya upinzani.

Joseph Kabila, rais wa sasa ambaye yuko madarakani tangu mwaka 2001, alitangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 49, huku mpinzani wake wa karibu Etienne Tshisekedi akifuatia kwa asilimia 32.

Etienne Tshisekedi aliyepinga ushindi wa kabila na kujitangaza Rais mteule

Etienne Tshisekedi aliyepinga ushindi wa kabila na kujitangaza Rais mteule

Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, wakereketwa wa upinzani mjini Kinshasa walichoma moto matairi na kuwarushia mawe polisi mitaani. Polisi walijibu kwa mabomu ya kutoa machozi na kuwafyatulia risasi, na watu wanne ambao wanadaiwa kuwa waporaji waliuawa.

Etienne Tshisekedi aliyapinga matokeo hayo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi. Kuwepo kwa maelfu ya maafisa wa usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo kumezuia kutokea kwa fujo kubwa, lakini bado wingu la wasi wasi limetanda juu ya nchi hiyo katika kipindi cha kusubiri kufahamu namna mzozo huu utakavyosuluhishwa.

Wachambuzi wengi wameonya kuwa hali kufuatia uchaguzi huu ambao ni wa pili nchini humo baada ya vita vya mwaka 1996 hadi 2003, inaweza kulipuka na kusababisha umwagaji damu. Kanisa katoliki ambalo lilikuwa na wakala 30 elfu kufuatilia uchaguzi huu pia limeuwekea ushindi wa Joseph Kabila alama ya kuuliza.

Rais Joseph Kabila ameutetea ushindi wake, licha ya kukubali kuwa makosa kadhaa yalifanyika.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Abdul-RahmanMohammed

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com