1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waipatia Uhispania Euro bilioni 30

10 Julai 2012

Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro wamekubaliana kuipatia Uhispania mkopo wa euro bilioni 30, kusaidia mabenki ya nchi hiyo ambayo kwa sasa yanakumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha.

https://p.dw.com/p/15UW4
Mawaziri wa EU wakutana Brussels
Mawaziri wa EU wakutana BrusselsPicha: dapd

Mkopo huo kwa Uhispania umeafikiwa baada ya mkutano wa masaa wa mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro, ambao umemalizika usiku wa manane kuamkia leo. Jean Claude Juncker, mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri hao ambaye pia ni waziri mkuu wa Luxembourg, amesema kuwa makubaliano rasmi juu ya mkopo kwa Uhispania yanatazamiwa pia mwishoni mwa mwezi huu wa Julai.

''Tunatazamia kupata makubaliano rasmi mnamo nusu ya pili ya mwezi Julai, tukitilia maanani utaratibu wa mabunge ya nchi, katika kuruhusu kutolewa kwa sehemu ya kwanza ya mkopo ambao unafikia bilioni 30 mwishoni mwa mwezi, na kuwekwa tayari kuweza kusaidia ikiwa kutatokea sababu za dharura katika sekta ya mabenki ya Uhispania.'' Amesema Juncker.

Jean Claude Juncker, mwenyekiti wa mikutano ya mawaziri wa fedha wa EU
Jean Claude Juncker, mwenyekiti wa mikutano ya mawaziri wa fedha wa EUPicha: Reuters

Juncker aongezewa muda wa uongozi

Jean Claude Juncker ambaye amekuwa mwenyekiti wa mikutano ya mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro tangu mwaka 2005, jana aliteuliwa tena na mawaziri kuendelea na wadhifa huo.

Uhispania ambayo imeshuhudia kiwango cha riba inayotozwa kwenye mikopo kikiongezeka sana kutokana na wasiwasi wa masoko, mwezi Juni iliomba kupatiwa msaada wa euro bilioni 100.

Mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro pia wameiongezea Uhispania muda wa hadi mwaka 2014 kufikia nakisi ya bajeti ya 3.0 kwa kuzingatia jinsi uchumi wake ulivyo katika hali ngumu kwa sasa.

Hata hivyo, Jean Claude Juncker amesema ni lazima Uhispania itekeleze hatua zinazohitajika kuupa uchumi wake sura inayoendana na viwango vya Umoja wa Ulaya. Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya kiuchumi Olli Rehn amesema nakisi katika bajeti ya Uhispania kwa sasa iko kwenye asilimia 6.3 na inatarajiwa kushuka hadi asilimia 4.5 mwaka 2013.

Hatua za kupunguza nakisi ni muhimu

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ameahidi kupunguza nakesi katika bajeti ya nchi
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ameahidi kupunguza nakesi katika bajeti ya nchiPicha: AP

Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy alisema jana kuwa angechukua hatua za ziada kupunguza nakisi katika bajeti ya taifa, na kuutaka Umoja wa Ulaya kutimiza mara moja ahadi zake. Uteuzi mwingine muhimu walioufanya mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro ni ule wa mjerumani Klaus Regling, mwenyekiti wa mfuko wa uokozi ujulikanao kama EFSF, kuwa mwenyekiti wa fuko jipya liitwalo ESM.

EFSF, ambalo ni fuko la kuhakikisha utengamano wa kifedha barani Ulaya ilianzishwa mwaka 2010 baada ya kutoa mkopo wa kuunusuru uchumi wa Ugiriki, lakini baadaye ilibainika kuwa hata Ureno na Jamhuri ya Ireland pia zingehitaji msaada. ESM kwa upande mwingine ina euro 500 katika akaunti yake, na inalo jukumu la kuwekeza moja kwa moja katika bajeti.

Waziri wa Ufaransa Pierre Moscovici alisema kuwa mkutano wao ulifikia maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na kuweka ratiba maalum inayoendelea hadi mwisho wa mwaka. Maazimio ya mkutano huu wa mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro yatawasilishwa katika mkutano wa mawaziri kutoka nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya, ambao watafanya tathmini ya ya hali ilivyo kwenye masoko, ili kuweka ramani ya njia wanayopaswa kufuata.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef