1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waafikiana juu ya mabenki

13 Desemba 2012

Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano juu ya kuipa Benki Kuu ya Ulaya mamlaka ya kuyafanyia ukaguzi mabenki ya nchi wanachama. Makubaliano hayo ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye ushirikiano wa kuiimarisha sarafu ya Euro.

https://p.dw.com/p/171Wd
Makubaliano kuhusu Euro
Makubaliano kuhusu EuroPicha: picture-alliance/dpa

Makubaliano hayo kuipa Benki Kuu ya Ulaya mamlaka ya kuzikagua benki zaidi ya 150 zilizo katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro, yamefikiwa baada ya mazungumzo magumu ya saa 14, yaliyowahusisha mawaziri wa fedha wa nchi zote 27 zinazounda Umoja wa Ulaya. Kulingana na mamlaka hayo, Benki Kuu ya Ulaya itakuwa ikiyafanyia ukaguzi wa moja kwa moja mabenki hayo makubwa, na kuingilia kati katika mabenki madogo zaidi ikiwa kutakuwa na dalili za matatizo.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier ameueleza mkutano wa mawaziri hao kwamba hakuna utata wowote juu ya ukweli kwamba kuanzia sasa Benki Kuu ya Ulaya itakuwa na mchango muhimu.

Makao makuu ya Benki Kuu ya Ulaya mjini Frankfurt
Makao makuu ya Benki Kuu ya Ulaya mjini FrankfurtPicha: Johannes Eisele/AFP/GettyImages

Nidhamu na uwajibikaji

Akizungumza kabla ya makubaliano hayo kufikiwa, Rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso amesema suala la nidhamu na uwajibikaji ni muhimu katika kumaliza mgogoro wa madeni unaoikabili kanda inayotumia sarafu ya Euro.

''Tunalazimika kuhakikisha kwamba masuala ya nidhamu na uwajibikaji yanakwenda sambamba. Tunahitaji mshakamano na maridhiano, hatuwezi kuchagua kati mshikamano na uwajibikaji.'' Alisema Barroso.

Majukumu ya Benki Kuu ya Ulaya kuanza kuyakagua mabenki yataanza rasmi tarehe 1 Machi mwaka 2014, baada ya mazungumzo na Bunge la Ulaya. Hata hivyo, mawaziri wamesema kuanza kwa jukumu hilo kunaweza kucheleweshwa iwapo Benki Kuu ya Ulaya itaomba muda zaidi kufanya maandalizi.

Mpango huu unaashiria mabadiliko makubwa kabisa kuliko yote yaliyofanyika katika benki za Ulaya tangu kuanza kwa mzozo wa kifedha mwaka 2007. Sasa hivi mpira umerushwa kwa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya ambao wanakutana mjini Brussels kwa siku mbili kuanzia leo, kuupa mpango huo uungaji mkono kisiasa.

Mawaziri wa fedha wa Ufaransa na Ujerumani, Pierre Moscovici na Wolfgang Schäuble
Mawaziri wa fedha wa Ufaransa na Ujerumani, Pierre Moscovici na Wolfgang SchäublePicha: Reuters

Schäuble alegeza msimamo

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amegeuza msimamo na kuachana na upinzani wake kuhusu jukumu la Benki Kuu ya Ulaya kuyafanyia ukaguzi mabenki, ambao ulimfanya afarakane wazi wazi na mwenzake wa Ufaransa Pierre Moscovici.

Pande hizo mbili zimekubali kuridhiana ili kuweza kupata makubalianao kabla ya mwaka kumalizika, kwa kukubali matakwa ya Ujerumani kutaka viongozi wa baraza la usimamisi la Benki Kuu ya Ulaya wawajibike kujibu maswali kuhusu namna ukaguzi unavyoendeshwa.

Makubaliano haya ya ukaguzi wa pamoja wa mabenki ni hatua muhimu katika kukabiliana na matatizo yanayoyakumba mabenki, ambayo mnamo miaka ya hivi karibuni yalitishia kuziweka nchi kama Uhispania na Ireland katika hali mbaya.

Mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuruhusu kutolewa kwa awamu ya mwisho ya mkopo wa Euro bilioni 34.4 kwa Ugiriki, kuisaidia nchi hiyo kupunguza matatizo makubwa yanayouzonga uchumi wake.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPA

Mhariri: Josephat Charo