1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kushirikiana na mataifa ya Balkan

Sylvia Mwehozi
17 Mei 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wenzao kutoka nchi za magharibi mwa Balkan wamezisifu hatua mpya za ushirikiano na ukanda huo wakati walipokutana katika mji mkuu wa Bulgaria wa Sofia.

https://p.dw.com/p/2xtUd
Der mazedonische Ministerpräsident Zoran Zaev mit der deutschen Kanzlerin Angela Merkel in Sofia
Picha: Government Macedonia

Mkutano wa kwanza wa kilele baina ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya magharibi mwa Balkan katika kipindi cha miaka 15 haukujadili moja kwa moja nyongeza ya mataifa hayo sita ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Serbia, Bosnia, Montenegro, Kosovo, Macedonia na Albania, lakini hasa ulilenga kwenye uwekezaji na ushirikiano.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayehudhuria mkutano huo amesema kwamba. "Leo tumezungumzia masuala ya mataifa ya magharibi mwa Balkan. Boyko Borissov amelifanyia kazi kwa kina na ni maslahi yetu sote, nia ya kulinda amani na usalama ili tuwe na kanda ya Balkan iliyo salama na maendeleo ya uchumi madhubuti na ndio sababu nina furaha kuangazia mazungumzo yajayo".

Bulgarien EU-Balkan-Gipfel in Sofia | Merkel & Vucic
Kansela Merkel na baadhi ya viongozi wa nchi za BalkanPicha: picture alliance/AP Photo

Katika barua yake kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kuelekea mkutano wa leo, rais wa baraza la Umoja huo Donald Tusk amesema ushirikiano wa kanda hiyo na Umoja wa Ulaya ni uwajibikaji wa pande zote.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema Umoja wa Ulaya umekuwa ukitoa "mtazamo mdogo sana" kwa mataifa ya magharibi mwa Balkan katika miaka ya karibuni, ambayo ni muhimu kwa kanda hiyo na muungano wa Ulaya.

Waziri mkuu wa Croatia Andrej Plenkovic amesema pengo la miaka 15 ya mkutano wa ngazi ya juu kama huo limekuwa kubwa sana, akibainisha kuwa Umoja wa Ulaya na viongozi wa kanda ya Balkan wamepanga kukutana tena mwaka 2020 ili kutoa usaidizi unaoonekana kwa ukanda huo.

Wakati wa mkutano huo wa kilele Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuthibitisha kwamba utawekeza katika miundombinu ili kuongeza ushirikiano baina ya kanda hiyo na muungano wa Ulaya.

Bulgarien EU-Westbalkan-Gipfel in Sofia
Viongozi wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa mjini SofiaPicha: Reuters/S. Nenov

Naye waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amesema nchi yake itajiondoa katika Umoja wa forodha pale itakapoondoka katika muungano wa Ulaya lakini vyanzo vinasema London ilikuwa ikizingatia kuomba ushuru wa nje wa Umoja huo kwa kipindi cha zaidi ya Desemba 2020.

Alipoulizwa na waandishi wa habari pembezoni mwa  mkutano wa kilele mjini Sofia kuhusu ripoti kwamba London itaomba kusalia katika umoja wa forodha baada ya kipindi cha mpito cha baada ya Brexit, May amekanusha kusuasua juu ya mipango hiyo ya kuondoka.

"Hapana Uingereza itaondoka umoja wa forodha, tunapoondoka Umoja wa Ulaya. Bila shaka tutajadiliana mipango ya baadae ya forodha na Umoja wa Ulaya."

Waziri huyo mkuu amesema malengo ya Uingereza ni kuwa na sera yake ya biashara na ulimwengu wote, uwepo wa biashara isiyo na misuguano na Umoja wa Ulaya na "hakutokuwa na ugumu wa mipaka" na mwanachama wa Umoja wa Ulaya Ireland.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman