1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yahitaji mshikamano - Juncker

14 Septemba 2016

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, ametowa mwito wa kuwepo ushirikiano na mshikamano miongoni mwa nchi za Umoja huo akisistiza kwamba hauwezi kusambaratika licha ya kuwepo mivutano.

https://p.dw.com/p/1K1m8
Jean-Claude Juncker, mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya
Jean-Claude Juncker, mkuu wa halmashauri ya Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Juncker ametoa kauli hiyo katika hotuba muhimu ya kwanza kuhusu sera za Umoja huo tangu Uingereza ilipoamua kujitenga na chombo hicho.

Hotuba hiyo ya Juncker imelenga kuweka wazi kwa mara ya kwanza tangu Uingereza ilipopiga kura ya kujitoa katika Umoja huo mipango kabambe ya Umoja huo, ambapo amesema uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya ni sawa na onyo kwamba Umoja huo unakabiliwa na mapambano ya kufa kupona dhidi ya siasa kali za utaifa zinazoshuhudiwa katika kila nchi ya Umoja wa Ulaya.

Katika bunge la Umoja huo mjini Strasburg, Juncker amesema hakuna umoja wa kutosha ndani ya Umoja wa Ulaya na badala yake kilichopo ni migawanyiko na mtengano ambayo inakiacha chombo hicho kutoa nafasi ya kushamiri kwa wasiotaka kukiona kikishikamana.

Lakini pamoja na ukweli huo, mkuu huyo wa Umoja ww Ulaya, amesisitiza pia kwamba anaamini jumuiya hiyo ya kibiashara yenye nguvu duniani bado ina umuhimu mkubwa na kwamba haipo hatarini.

Bunge la Ulaya-Straßburg Ufaransa
Bunge la Ulaya-Straßburg UfaransaPicha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

"Ikiwa tunataka kuimaliza migawanyiko kati ya mashariki na Magharibi iliyoongezeka katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni na ikiwa tunataka kuuonesha ulimwengu kwamba Ulaya bado ni chombo kinachoweza kuchukua uamuzi wa pamoja tunabidi tufanye kazi'."

Kadhalika, mkuu huyo wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema litakuwa jambo la busara endapo ombo la Uingereza kujitoa litafanyika haraka iwezekanavyo ili kufanikisha hatua zinazohitajika kuchukuliwa baada ya hapo.

Juu ya hilo pia amegusia kwamba uhusiano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya utabidi kubakia katika misingi ya kirafiki, na pia kuchukua mwelekeo mpya ikiwa ni pamoja na mageuzi katika suala zima la soko huru la ndani ya jumuiya hiyo.

Kuna khofu kwamba Umoja huo wa Ulaya unakabiliwa na mkwamo hadi pale Uingereza itakapoamua kuchukua hatua katika suala zima la Brexit. Kujiondoa kwa Uingereza kumeongeza mashaka na hali ya kuvunjika moyo katika nchi 27 zilizobakia katika Umoja wa Ulaya pamoja na viongozi wake ambao watakutana ijumaa huko Bratislava kutafakari jinsi ya kuendelea mbele.

Kwa upande mwingine Junker ametowa mwito pia wa kuwepo mshikamano miongoni mwa nchi hizo za Umoja wa Ulaya kuhusu mgogoro wa wakimbizi.

Wahamiaji kutoka Libya
Wahamiaji kutoka LibyaPicha: picture alliance/AP Photo/E. Morenatti

Linapokuja suala la kulimudu suala la mgogoro wa wakimbizi tumeanza kuona mshikamano naamini mshikamano zaidi unahitajika lakini pia tufahamu kwamba mshikamano unabidi ufanyike kwa khiari na hauwezi kulazimishwa.

Sambamba na hilo ametaja kwamba Umoja wa Ulaya utakuwa unakwenda kinyume na maadili ya historia yake ikiwa itashindwa hivi leo kuwalinda watoto wanaowasili barani humo baada ya kutoroka nchi zinazokabiliwa na vita Mashariki ya Kati na Afrika.

Mwandishi: Saumu Yussuf/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef