1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuafikiana na Uturuki kuhusu wakimbizi

18 Machi 2016

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kufikia muafaka muhimu na Waziri Mkuu wa Uturuki wa kuutatua mgogoro wa wahamiaji baada ya kukubaliana kuhusu msimamo wa pamoja katika mkutano wa kilele mjini Brussels

https://p.dw.com/p/1IFb9
Belgien EU-Gipfel Angela Merkel Lars Lokke Rasmussen und Mark Rutte
Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk anawasilisha mapendekezo hayo yenye utata kwa Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu, ambayo Uturuki itatakiwa kuwapokea wahamiaji wote na wakimbizi wanoingia kutokea Ugiriki, kabla ya kushiriki katika mkutano na viongozi wote 28 wa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu amesema mpango huo unaopendekezwa ni wa wazi na kuaminika lakini akaongeza kuwa Utruruki haitawahi kuwa gereza la wazi kwa wahamiaji. Ulaya inautegemea muafaka huo kupunguza wimbi kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa la wahamiaji milioni 1.2 tangu mwanzo wa mwaka wa 2015, linalosababishwa na vita vya Syria, lakini Uturuki itatangaza gharama kubwa kabla ya kukubali mpango huo. Licha ya wasiwasi katika mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya kuhusu rekodi ya haki za binaadamu ya Uturuki, nchi hiyo imedai kuharakishwa kwa jaribio lake lililokwama kwa muda mrefu la uwanachama wa Umoja wa Ulaya, kupewa msaada zaidi wa mabilioni ya euro na kukubaliwa kuwa na usafiri huria.

Griechenland Mazedonien Flüchtlinge bei Idomeni
Wahamiaji wakiwa njiani kuelekea Macedonia kutoka kambi ya wakimbizi ya Idomeni, UgirikiPicha: Getty Images/M. Cardy

Kansela wa Ujerumani amesema mpango huo ni fursa nzuri ya kuzuia biashara ya wasafirishaji watu. "Masharti kadhaa yatastahili kuwekwa kwa ajili ya ulinzi wa wakimbizi kulingana na viwango vya kimataifa. Hii ni sehemu ya mkakati huo, na ili kuwa na usafiri huria bila Visa, viwango Fulani vya sheria ya kimataifa lazima vishirikishwe katika sheria ya Uturuki ikiwa hilo halijafanyika tayari".

Wakosoaji pia wameibua wasiwasi kuwa muafaka huo huenda ukakiuka sheria za kimataifa ambazo zinazuia kufukuzwa kwa jumla kwa wakimbizi.

Mgogoro wa wahamiaji umeendelea kuigawa Ulaya, wakati kukiwa na hofu kuwa mkataba wake wa Schengen wa usafiri huria huenda ukavunjika kwa sababu mataifa wanachama yataweka uthibiti wa mipaka na pia kuchipuka kwa vyama vinavyotafuta umaarufu kupitia hisia za kupinga uhamiaji.

Lakini baadhi ya viongozi wa Ulaya wameelezea wasiwasi kuwa muafaka huo – ambao Umoja wa Ulaya utamchukua mkimbizi mmoja wa Kisyria kutoka ardhi ya Uturuki kwa kubadilishana na kila Msyria atakayechukuliwa tena na Uturuki kutokea Ugiriki – huenda ukawa kinyume cha sheria.

Lengo la mpango huo ni kuwahimiza Wasyria kuomba hifadhi katika Umoja wa Ulaya wakati wakiwa wangali kwenye ardhi ya Uturuki, badala ya kuhatarisha maisha kwa kutumia maboti ya wasafirishaji haramu wa watu katika Bahari ya Aegean. Muafaka huo pia utaipa msaada muhimu Ugiriki ambako maelfu ya wakimbizi wamekwama katika mazingira duni baada ya nchi za Balkan kufunga mipaka yao na kuwazuia kuingia Ujerumani na nchi za Skendinevia

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo