1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine imeanza kulipa deni lake la gesi kwa Urusi

Mjahida2 Juni 2014

Urusi imethibitisha kuwa Ukraine imeanza kulipa awamu ya kwanza katika mfululizo wa malipo kwa ajili ya gesi yake

https://p.dw.com/p/1CARZ
Bomba la gesi inayosafirishwa kutoka Urusi
Bomba la gesi inayosafirishwa kutoka UrusiPicha: Reuters

Hii ni mojawapo ya suala lililoeneza wasiwasi kati ya nchi hizi mbili.

Aidha shirika la habari la Interfax limeinukuu wizara ya nishati nchini Urusi ikisema kwamba takriban dola Milioni 786.4 imelipwa na msambazaji wa gesi ya Naftogas nchini Ukraine kama hatua ya kwanza ya kulipia madeni yake kwa Urusi.

Hata hivyo Urusi imesema inaidai Ukraine jumla ya dola bilioni 5.2 kutokana na gesi iliokuwa inatolewa kwa nchi hiyo. Urusi ilikuwa imetishia kusimamisha mtiririko wa gesi hiyo iwapo deni lake halitalipwa. Mazungumzo mapya juu ya ulipaji huo yanatarajiwa kufanyika tena hii leo mjini Brussels.

Mapigano bado yanaendelea mjini Luhansk

Huku hayo yakiarifiwa mapigano makali yanaendelea katika eneo lililo na waasi Mashariki mwa Ukraine baada ya waasi waliotiifu kwa Urusi kuushambulia mpaka wa Ukraine kwa mabomu mapema hii leo asubuhi.

Kulingana na maafisa wa usalama kikosi cha waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine walilivamia ghorofa ya juu ya jengo moja mjini Luhansk, mji ulio karibu na Urusi, na kuanza kushambulia kwa risasi eneo la mpakani.

Baadhi ya Waasi wanaotaka kujitenga
Baadhi ya Waasi wanaotaka kujitengaPicha: ap

Msemaji wa mpakani Oleh Slobodin amesema watu watano wameuwawa huku wengine wanane wakijeruhiwa.

Eneo la Mashariki mwa Ukraine limekuwa likikaliwa na waasi wenye silaha wanaotaka kujitenga kwa takriban miezi miwili iliopita, ambapo serikali ya Ukraine inadai Urusi ndio iliounda kundi hilo la waasi.

Serikali hiyo imeongeza kuwa wapiganaji wa Ukraine na wale wa kutoka eneo la Caucasus wameungana pamoja na waasi kuupiga vita utawala wa Kiev.

Urusi kuwasilisha Mswada wa azimio kwa UN

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema nchi yake itawasilisha mswada wa azimio lake kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kutaka kusimamishwa mara moja ghasia nchini Ukraine na pia kuundwa kwa njia salama Mashariki mwa Ukraine zitakazotumiwa na raia kukimbia maeneo yaliokumbwa na vita.

"Tunataka Umoja wa Mataia uhakikishe hakuna vizuizi vyovyote vitakavyowekwa kuzuia raia kuondoka katika maeneo yalio na oparesheni za kijeshi au kuzuwiya kutolewa kwa misaada ya kibinaadamu katika maeneo hayo," Alisema Lavrov.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: REUTERS

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Waziri huyo wa mambo ya nchi za kigeni wa Urusi alisema mataifa ya Magharibi yaliihakikishia kwamba hali itaimarika nchini Ukiraine baada ya uchaguzi wa Mei 25, lakini hali inazidi kusambaratika.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman