1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Wingu lagubika makubaliano ya amani wakati wa Ramadhan, Gaza

Lilian Mtono
10 Machi 2024

Mapigano makali yameugubika Ukanda wa Gaza hii leo huku kukiwa hakuna ishara ya makubaliano ya kusimamishwa ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

https://p.dw.com/p/4dMTG
Mzozo wa kibinaadamu unazidi kuitikisa Gaza kutokana na vita
Wapalestina wakiwa wamekusanyika kwenye ufuo wa bahari kwa matumaini ya kupata msaada wa chakula unaoangushwa na ndege huko Gaza, wakati mapigano yakiendelea kati ya Israel na Hamas, kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Meli ya misaada ya Uhispania iliyobeba chakula inatarajiwa kuondoka Cyprus hivi karibuni kwa ajili ya kusafirisha misaada hiyo inayolenga kupunguza mateso kwa watu wa Gaza wanaokabiliwa na vita kwa mwezi wa sita sasa.

Kundi lisilo la kiserikali la Open Arms linaloshirikiana na shirika la misaada la Marekani la World Central Kitchen, limesema meli hiyo iliyobeba tani 200 za vyakula, litavishusha katika pwani za Gaza ambako imejenga bandari ndogo.

Katikati ya hofu ya janga la njaa katika baadhi ya maeneo yaliyozingirwa ya Gaza, ndege kutoka Marekani, Jordan na kwingineko zimekuwa zikidondosha vyakula vya misaada, lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kwamba haviwatishi watu milioni 2.4 wa eneo hilo.