Ujerumani yatimiza miaka 50 ya kuendeleza michezo duniani | Masuala ya Jamii | DW | 05.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Ujerumani yatimiza miaka 50 ya kuendeleza michezo duniani

Mwezi huu wa Januari 2011 Shirika la Kuendeleza Michezo la Ujerumani linaadhimisha miaka 50. Tangu mwaka 1961 shirika hili limekuwa likishughulika na miradi ya uendelezaji michezo katika nchi zinazoendelea.

Muogeleaji wa masafa marefu

Muogeleaji wa masafa marefu

Chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, wataalamu wa michezo wa Kijerumani wamekuwa wakifanya kazi ulimwengu mzima kuwafundisha vijana wa nchi zinazoendelea michezo na mazoezi.

Jambo hili limesaidia sana kuimarisha mahusiano na maingiliano baina ya tamaduni tafauti, maana michezo huibua mambo mengine pia, kama vile elimu, ushirikiano na uwezo wa kujitegemea. Ndivyo yalivyo maoni ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Cornelia Pieper, ambaye anaamini kuwa kwa kufanya hivi, Ujerumani imekuwa ikiendeleza sio tu michezo, bali pia uadilifu, ustahamilivu, ushindani na maelewano.

"Michezo ni muhimu sana, pia kwa uwezo wa watu kujtegemea na kwa vijana kujiendeleza. Kwa hivyo tunaweza kujiwekea malengo ya kuifikia." Anasema Pieper.

Haya mtu anaweza kuyachukulia kuwa malengo makubwa mno ya kisiasa katika michezo, lakini Ralph Mouchbahani, ambaye amekuwa mwalimu wa riadha kwa miaka 30 sasa, anasema hilo linawezekana, kwani ili kuweza kujenga mifumo ya kijamii na mahusiano baina ya watu, "michezo ina nafasi kubwa zaidi."

Na mifano iko ya kutosha. Mpira wa miguu wa wanawake nchini Afghanistan, mpira wa watu wenye ulemavu nchini Cambodia au Senegal. Euro milioni tano hutumika kila mwaka kwenye Wizara ya Mambo ya Nje kwa ajili ya kugharamikia michezo kwenye nchi zinazoendelea.

Timu ya wanawake ya Iran

Timu ya wanawake ya Iran

Wizara hii imekuwa ikishirikiana na Kamati ya Olimpiki ya Ujerumani, kuanzisha miradi ya vituo vya kufundishia mpira wa miguu na riadha. Tangu mwaka 1961 hadi sasa, zaidi ya wanamichezo 1300 wameshafaidika na miradi hii. Katrin Merkel, ambaye ni mkuu wa Kamati ya Olimpiki, anasema kwamba wao huwa hawaipuizii nchi yoyote. Hata katika nchi ambazo uhusiano wa kidiplomasia haufanyi kazi vyema, "michezo huwa njia nzuri zaidi."

Hata hivyo, kuna mipaka. Mfano halisi ni Sudan, ambako kutokana na kutokuwepo na uhakika wa mustakabali wa kisiasa, hakuna mradi wa kuendeleza michezo unaofanyika huko, lakini Merkel asema hilo ni jambo la kisehria.

"Mamlaka yetu hayatoki nje ya sheria. Miradi haitakiwi kuingilia maslahi ya kisiasa ya maeneo husika." Anasema Merkel.

Hapana shaka, jukumu la kuendeleza michezo duniani limekuwa na ugumu wake. Si kila wakati matarajio ya wanaofundishwa na wanaofundisha hufikiwa. Kimsingi, majukumu ya wataalamu wa michezo ni makubwa: hawatakiwi tu kuwa wakufunzi wa michezo, bali pia wanataaluma na wanadiplomasia, wenye uelewa na ufahamu mkubwa wa mambo.

Na lazima, kwa hivyo, wapatiwe mafunzo maalum na wafanyiwe tathmini ya kutosha kila baada ya kukamilika kwa mradi. Ni pale tu wanapokuwa wameweza kuufikisha ujumbe wa Ujerumani kupitia michezo, ndipo ambapo wanakuwa wamefanikiwa kuwasaidia wanamichezo wa jamii zinazoendelea ili nao wajisaidie wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Felix Hoffmann

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 05.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztyF
 • Tarehe 05.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztyF

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com