Ufaransa yainyuka Ujerumani
14 Novemba 2015Mabingwa hao wa kombe la dunia Ujerumani waliteleza kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wa fainali za mwakani za kombe la mataifa ya Ulaya Ufaransa katika mchezo ambao uligubikwa na shambulio la risasi mjini Paris pamoja na miripuko karibu na uwanja wa Stade de France, wakati Uhispania nayo ikainyoa Uingereza kwa mabao 2-0 katika usiku wa michuano hiyo ya kirafiki.
Ubelgiji ikishika nafasi ya kwanza katika orodha ya FIFA ya timu bora kwa sasa iliishinda Italia kwa mabao 3-1, wakati Uholanzi iliyoshindwa kufuzu kucheza fainali za mwakani za kombe la mataifa ya ulaya , iliibwaga Wales iliyofanikiwa kukata tikiti ya fainali hizo kwa mabao 3-2.
Na michezo mingine kwingineko , Poland iliishinda Iceland kwa mabao 4-2, Slovakia ikashinda mpambano wake dhidi ya Uswisi kwa mabao 3-2, Jamhuri ya Cheki ikawa mshindi dhidi ya Serbia kwa mabao 4-1, Ireland ya kaskazini ikaitungua Latvia kwa bao 1-0, Uturuki ikaishinda Qatar kwa mabao 2-1 na Luxemburg ikaishinda Ugiriki kwa bao 1-0.
Kipigo baada ya michezo 16
Uingereza ilijikuta ikipokea kipigo chake cha kwanza katika michezo 16 kwa mabao 2-0 dhidi ya wabingwa watetezi wa kombe la mataifa ya Ulaya Uhispania mjini Alicante.
"Tulicheza dhidi ya timu nzuri sana. Ilikuwa hali tuliyoitarajia," kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema.
Mchezaji wa kati wa Uhispania Cesc Fabregas amesema : " tulistahili, tumecheza kandanda safi. Tulishambulia kila wakati."
Wahanga wa Heysel wakumbukwa
Mjini Brussels , mchezo wa kirafiki kati ya Ubelgiji na Italia ulisimamishwa katika dakika ya 39 na kukaa kimya kwa muda wa dakika moja kuwakumbuzka wahanga 39 raia wa Italia waliofariki katika ajali iliyotokea katika uwanja wa Heysel miaka 30 iliyopita.
Shambulio baya mjini Paris liligubika mchezo muhimu wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani uliohudhuriwa na rais Francois Hollande wa Ufaransa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ambapo baadaye rais wa Ufaransa alitangaza amri ya hali ya hatari na kusema anafunga mipaka ya nchi hiyo.
Miripuko ilisikika ndani ya uwanja wa stade de France katika kitongoji cha St Denis, kaskazini ya Paris, ambako fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya mwakani itafanyika. Mabao ya Ufaransa yalitiwa kimiani na Oliver Giroud na Andre-Pierre Gignac.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri:Gakuba Daniel