1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaidhinisha ndoa za jinsia moja

Admin.WagnerD30 Juni 2017

Bunge la Ujerumani limepiga kura kuruhusu ndoa za watu wa jinsia moja baada ya Kansela Angela Merkel kubadili msimamo kuruhusu wanachama wa kundi lake la kihafidhina kufuata imani zao badala ya msimamo wa chama.

https://p.dw.com/p/2fgnp
Deutschland Bundestag Abstimmung über Ehe für Alle
Picha: REUTERS/F. Bensch

"Kwangu mimi ndoa katika Sheria ya Msingi ni ndoa kati ya mwanaume na mwanamke na ndio sababu sikupiga kura ya kuunga mkono  muswada huu leo hii.Ni kweli hicho kilichosemwa katika mdahalo wa leo. Ulikuwa ni mdahalo uliochukuwa muda mrefu ni mzito na kwa wengi yalikuwa majadiliano yenye hisia nzito.Jambo hili pili limenigusa mimi mwenyewe binafsi.Ndio sababu natumai kura hii leo hii sio tu inakuza heshima baina ya maoni tofauti bali pia inaleta maelewano zaidi ya kijamii na amani.Asante."

Kauli hiyo ameitowa Merkel anayewania muhula wa nne madarakani katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Septemba 24 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya uamuzi huo wa kihistoria  ulioidhinisha ndoa ya watu wa jinsia moja nchini Ujerumani ambapo binafsi amepiga kura ya kuukataa kwa sababu anaamini kwamba ndoa ni kama inavyoelezewa na sheria ya Ujerumani ni kati ya mwanaume na mwanamke.

Lakini amesema uamuzi wake huo ni wa binafsi na kuongeza kwamba amezidi kupata imani miaka ya hivi karibuni kwamba wana ndoa wa jinsia moja wanapaswa kuruhusiwa kusaili watoto.

Kura 393 zaunga mkono didi ya 226

Deutschland Demonstranten vor dem Bundestag  während die Delegierten über die Legalisierung gleichgeschlechtlicher Ehe in Berlin abstimmen
Watu wakisheherekea mbele ya bunge la Ujerumani baada ya kuidhinishwa kwa ndoa za watu wa jinsia moja.Picha: REUTERS/H. Hanschke

Nobert Lambert Spika wa bunge la Ujerumani amesema wabunge 393 wamepiga kura ya kuunga mkono ndoa ya jinsia moja wakati wabuge 226 wamepiga kura ya kupinga na wabunge wanne hawakupiga kura.

Nchi nyengine nyingi za Ulaya ikiwemo Ufaransa,Uingereza na Uhispania tayari zimehalalisha ndoa za jinsia moja.

Tangazo la Merkel alilolitowa hapo Jumatatu kwamba atawaruhusu wabunge kupiga kura juu ya ndoa ya jinsia moja kwa kuzingatia imani zao binafsi limewakera baadhi ya wabunge wanaounda muungano wake wa kihafidhina ambao kwa jadi umekuwa chini ya msingi wa Kikatoliki.

SPD yauona huo ni ushindi kwao

Deutschland Bundestag Abstimmung über Ehe für Alle
Mkuu wa kundi la wabunge wa SPD bungeni Thomas Oppermann.Picha: REUTERS/F. Bensch

Kura hii ya leo inaadhimisha ushindi wa nadra kwa chama cha Social Demokrat (SPD) ambacho ni mshirika wa Merkel katika serikali yake ya mseto ambacho kiko nyuma ya wahafidhina kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni.

Thomas Opperman mkuu wa kundi la wabunge wa chama  cha SPD bungeni amesema 

"Kwamba leo tunaamuwa tu pengine sio kitu kizuri kwa serikali ya mseto lakini ni jambo zuri kwa wananchi."

Chama hicho cha SPD kimetumia fursa ya tamko la kushangaza la Merkel alilolitowa Jumatatu kwao wao kusema kwamba watashinikiza kupigwa na mapema kwa kura hiyo ya kuidhinisha ndoa za jinsia moja nchini Ujerumani.

Lakini wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba suala hilo yumkini litakuwa limefifia kwenye mawazo ya wapiga kura utakapofika wakati wa uchaguzi mkuu hapo mwezi wa Septemba.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters

Mwandishi: Yusuf Saumu