1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaongoza juhudi mpya kwa Somalia

Admin.WagnerD23 Februari 2012

Mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia umeanza (23.02.2012) mjini London Uingereza, kujaribu kupata suluhisho kwa migogoro inayoikumba nchi hiyo ya pembe ya Afrika kwa zaidi ya miongo miwili.

https://p.dw.com/p/1485D
Mji mkuu wa Somalia ulioharibiwa na vita
Mji mkuu wa Somalia ulioharibiwa na vitaPicha: picture alliance/dpa

Mkutano huo unahudhuriwa na wawakilisha kutoka pande zenye ushawishi mkubwa duniani, zikiwemo nchi na mashirika ya kimataifa. Miongoni mwa washiriki ni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hilary Clinton, na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon. Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia wanashiriki katika mkutano huo.

Kitisho kinachovuka mipaka

Uingereza ambayo ndiyo muandalizi wa mkutano huo imesema lengo ni kupata suluhisho la kisiasa litakalopelekea kwenye amani ya kudumu nchini Somalia, na kuondoa kitisho kwa jamii ya kimataifa.

Tangazo lililotolewa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo limesema kwamba washiriki watatafakari hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa kusaidia mchakato wa amani kwa Somalia. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ndiye atakayeufungua rasmi mkutano huo. Cameron alisema kitisho cha Usalama nchini Somalia kinakwenda nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema ukosefu wa usalama Somalia ni kitisho kinachovuka mpaka
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema ukosefu wa usalama Somalia ni kitisho kinachovuka mpakaPicha: dapd

''Nadhani kuna kitisho kwa usalama ambacho ni dhahiri; ni kitisho kinachohamasisha matumizi ya nguvu katika kile kinachochukuliwa kama vita vitakatifu. Kitisho hicho hakiishii kwa Somalia pekee yake, kinavuka mipaka, na kuna hatari kubwa kwa vijana wa Uingereza wenye asili ya kisomali kuhadaiwa na vikundi vinavyofanya vita hivyo. Kwa hiyo ni kitisho cha ugaidi leo, na tusipokuwa makini kinaweza kuwa kikubwa zaidi baadaye.'' Alisema David Cameron.

Suala la uharamia wa baharini karibu na fukwe za Somalia kwenye bahari ya Hindi pia liko kwenye agenda ya mkutano huo.

Mohamed Ali Abdiweli, waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia
Mohamed Ali Abdiweli, waziri mkuu wa serikali ya mpito ya SomaliaPicha: Reuters

Enzi mpya yenye matumaini

Akizungumza na vyombo vya habari kwenye mkesha wa mkutano huo, waziri mkuu wa serikali ya mpito ya mjini Mogadishu, Abdiweli Mohammed Ali, alisema nchi yake inaelekea kwenye ''enzi mpya ya amani na utangamano''. Hata hivyo alikiri kutojua chochote juu ya uwezekano wa mkutano huu, kupendekeza msaada mkubwa kifedha kusaidia nchi yake kujijenga upya baada ya uharibifu wa vita vya muda mrefu.

Kiongozi wa jimbo la Puntland lililojitenga na Somalia, pamoja na kamanda wa kikundi cha Ahlu Sunna wal Jamaa kinachopinga al Shababu wamealikwa pia katika mkutano wa London, na jana walisaini makubaliano ya amani yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, kama ishara ya hatua nyingine mbele kwa Somalia.

Kikundi cha Al Shabab kinapinga mkutano huu wa London juu ya Somalia
Kikundi cha Al Shabab kinapinga mkutano huu wa London juu ya SomaliaPicha: AP

Pigo jingine kwa Al Shabab

Kikundi cha al shababu pia jana kilipata hasara kwenye uwanja wa mapambano, kwa kunyang'anywa mji muhimu wa Baidoa kufuatia mapigano makali kati yake na vikosi vya serikali ambavyo visaidiwa na majeshi ya Somalia. Al shababu, imesema mkutano wa London unalenga kuirudisha Somalia chini ya utawala wa kikoloni.

Marekani imesema inafikiria kuitisha vikwazo kwa watu ambao wanavuruga juhudi za maendeleo ya kisiasa nchini Somalia, miongoni mwao wakiwemo maafisa wa serikali ya mpito. Afisa mmoja wa nchi hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe, amewaambia wandishi wa habari kuwa vikwazo hivyo ni pamoja kuwanyima viza watu hao kusafiri nje ya nchi yao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman