1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari umo hatarini

3 Mei 2012

Leo (03.05.) dunia inaadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari lakini uhuru huo umo hatarini katika sehemu kadhaa za dunia.

https://p.dw.com/p/14oSO
Reporters without borders
Reporters without bordersPicha: dapd

Mapinduzi yayolitokea katika nchi za kiarabu na za kaskazini mwa Afrika yameleta mabadiliko ya kina kirefu katika nchi hizo, lakini haina maana kwamba kazi ya waandishi wa habari imekuwa rahisi. Msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wa habari wasiojali mipaka, kanda ya Ujerumani Michael Rediske ameeleza kuwa mapinduzi yaliyotokea katika nchi za kiarabu yamesababisha mgogoro mkubwa. Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa ugani, lakini aghalabu wanashambuliwa, hasa na serikali zao.

Hata hivyo viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vinatafautiana sana baina ya nchi na nchi. Kazi ya waandishi nchini Tunisia sasa siyo ya hatari kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini nchini Syria waandishi wa habari kadhaa wameuawa tokea mapigano yaanze nchini humo. Mazingira yanayowakabili waandishi wa habari nchini Syria leo ni hatari sawa na yale yaliyojiri nchini Iraq katika miaka ya nyuma.

Hakuna waandishi wa kujitegemea Korea Kaskazini

Akisisitiza umuhimu wa kuiadhimisha siku ya leo ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wasiojali mipaka , kanda ya Ujerumani bwana Rediske ameeleza: "Ni siku ya kutanabahisha juu ya matatizo, juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari, kwa kutilia maanani kwamba katika theluthi mbili ya nchi duniani, hakuna uhuru wa vyombo vya habari." Alitolea mfano wa Korea ya Kaskazini ambako hakuna waandishi wa kujitegemea, na kwa sababu hiyo hawakamatwi na Eritrea ambako waandishi wa habari wengi wanatiwa ndani.

Michael Rediske wa shirikia la waandishi wa habari wasiojali mipaka
Michael Rediske wa shirikia la waandishi wa habari wasiojali mipakaPicha: dapd

Katika sehemu fulani, katika nchi za kiarabu matarajio hayakutimizwa. Bwana Rediske ametoa mfano wa Misri. Amesema katika orodha iliyotolewa na asasi ya waandishi wasiojali mipaka Misri ipo katika maeneo ya mkiani kwa sababu watawala wa kijeshi wanatoa sheria zinayoubana uhuru wa vyombo vya habari.

Eritrea ni nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari

Asasi ya maripota wasiojali mipaka, kila mwaka inachapisha ripoti juu ya viwango vya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Ripoti ya mwaka huu inazihusu nchi 179. Wawakilishi wa shirika la waandishi wasiokuwa na mipaka walipata fursa ya kuzungumza na wanasayansi, wanasheria na w anaharakati wa kutetea haki za binadamu kutoka kila nchi.

Uhuru wa vyombo vya habari uliondolewa Eritrea miaka 10 iliyopita
Uhuru wa vyombo vya habari uliondolewa Eritrea miaka 10 iliyopitaPicha: AP Graphics

Kwenye mkia wa orodha ya nchi hizo 179 zipo nchi ambako hakuna kabisa uhuru wa vyombo vya habari au hauheshimiwi. Mfano ni Eritrea. Na siyo jambo la kushangaza, amesema Pierre Ambroise anaefuatilia maendeleo ya tasnia ya uandishi katika nchi za afrika kwa niaba ya shirika la waandishi wasiojali mipaka.

Amesema Eritrea ndiyo nchi ya hatari kuliko zote duniani kwa waandishi wa habari. Uhuru wa vyombo vya habari uliondolewa miaka 10 iliyopita. Wanaofanya kazi ni waandishi habari wa serikali wanaofuata maagizo ya wizara ya habari. Na yeyote anaeenda kinyume na maagizo hayo anaishia jela.

Lakini zipo habari za kutia moyo kutoka Afrika juu ya waandishi wa habari. Namibia na Cape Verde zimo miongoni mwa nchi 20 za mwanzoni ambako uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa. Tofauti na China ambako idadi kubwa ya waandishi wa habari wanatiwa ndani. Kwa mujibu wa shirika la waandishi wasiojali mipaka,hakuna nchi yenye idadi kubwa ya waandishi wa habari walofungwa kama China.

Mwandishi:Müller Marco

Tafsiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman