1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari Uganda

2 Mei 2007

Kesho ni siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari.Taasisi ya vyombo vya habari inayojulikana kama International Press Institute imetoa taarifa ya 2007 kuhusu hali ilivyokuwa mwaka jana mwaka jana wa 2006.

https://p.dw.com/p/CHF0
Bendera ya Uganda
Bendera ya Uganda

Nchi ya Uganda ilikuwa katika matatizo ya kisiasa na kiuchumi wakati Rais Yoweri Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986.Mabadiliko mengi yamefanyika tangu wakati huo ila katika nyanja za kisiasa yameshika kasi ndogo.Mwaka 2005 serikali iliamua kuruhusu vyama vya upinzani kuhusika katika siasa nchini humo.Katika upande wa haki za binadamu taarifa zinazoelezea visa vya uteswaji,ukosefu wa usalama katika eneo la kaskazini vilevile kuhangaishwa kwa wanasiasa wa upinzani zinashtumiwa vikali.

Hata hivyo vyombo vya habari vina uwezo kwa kiasi fulani kutangaza mijadala ya kisiasa.Hilo linadhihirishwa na zaidi ya magazeti 12 yanayochapishwa kila siku na kila wiki vilevile takriban vituo mia moja vya redio na televisheni ambavyo aghalabu hukosoa serikali.

Ada za juu za leseni za kuendesha vituo hivyo zimesababisha hali ngumu ya kiuchumi kwa vituo binafsi.

Katika miaka ya hivi karibuni hali nchini humo inazidi kuwa mbaya kwa mujibu wa wadadisi huku baadhi ya vituo wakibana taarifa wanazotangaza.

Kwa upande mwingine serikali imeweka sheria zinazowekea vikwazo shughuli za utangazaji kwa kisingizio cha kulinda usalama wa kitaifa. Jambo hili hasa hudhihirika wakati wa kutangaza matukio ya kisiasa ya kupinga serikali.Sheria ya uchochezi bado inatumiwa kuwashtaki waaandishi wa habari aidha wanahitajika kuwa na vibali na kutimiza masharti kadhaa.

Mwaka 2006 ulianza vibaya kwa waandishi wa habari.Baadhi ya waandishi wa habari walishtakiwa kwa kuandika taarifa tofauti tofauti wakati uchaguzi wa rais uliwadia huku Rais Museveni akiwaagiza kutotangaza kuhusu mada kadhaa ikiwemo jinsi upinzani unavyochukuliwa na serikali.

Serikali ilitumia mbinu kadhaa ili kuwatisha na kuwalazimisha waandishi wa habari kutotangaza katika kipindi hicho.Serikali ilizuia mtandao unaoukosoa vilevile matangazo ya kituo cha Radio Katwe wakati huo.

Mtandao wa Gazeti linaloongoza la kila siku la binafsi la The Monitor nao ulizuiwa huku matangazo ya kituo cha KFM kuingiliwa.Aidha serikali iliunda shirika jipya Media Centre la kutathmini kazi za waandishi na kwa upande mwingine kudhibiti idhini ya waandishi wa kigeni.Kulingana na Waziri wa Habari James Nsaba Buturo hatua hiyo ilichukuliwa kwasababu za kiusalama.Kwa mujibu wa baadhi ya waandisi wa kigeni shughuli ya usajili na kupata idhini ya kutangaza imekuwa ngumu zaidi huku muda wa vibali ukipunguzwa ikilinganishwa na awali.

Tarehe mosi mwezi wa Machi maafisa wa polisi walivamia kituo cha redio cha Choice kilicho mjini Gulu katika eneo la kaskazini la Uganda baada ya kukilaumu kuwa tishio la usalama .Kitendo hicho kilitokea baada ya kutangaza mahojiano na wagombea wa nafasi katika baraza la mji.Mahakama katika eneo hilo iliwakabidhi maafisa wa polisi hati ya kukamatwa wahusika na kuwaruhusu kukipekua kituo hicho cha redio.

Polisi hao walizuia mikanda ya sauti na kuamuru uongozi wa redio kuwakabidhi kibali chao cha kutangaza vilevile nakala ya kipindi kilichorushwa hewani.

Siku chache baada ya hapo msimamizi wa vipindi Martin Ojara Mapenduzi alikamatwa na kuzuiliwa usiku kucha bila shtaka lolote na kuachiwa baada ya kulipa dhamana.Mwezi machi tarehe 13 polisi walikifunga kituo hicho baada ya kutangaza makala iliyolikashifu jeshi na mwakilishi wa chama tawala cha NRM.

Kulingana na waraka wa Baraza la Uandishi nchini humo kitendo hicho kilikiuka sheria na vigezo vilivyowekwa vya utangazaji hivyo basi kuamuriwa kusimamisha matangazo kwa muda. Kwa uchache hivyo ni baadhi ya visa vya kukandamizwa kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda mwaka 2006