1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Uhaba wa mafuta wasitisha huduma za kibinaadamu Gaza

17 Novemba 2023

Umoja wa Mataifa umesitisha kwa siku moja siku ya Ijumaa uwasilishwaji wa misaada huko Gaza kutokana na hitilafu katika huduma za mawasiliano katika ukanda huo. Hayo ni kutokana na uhaba wa mafuta.

https://p.dw.com/p/4Z1Vg
Gaza Leben von Palästinensern im UNRWA-Lager in Khan Yunis
Mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa akisimamia msaada wa Chakula huko Gaza: 24.10.2023Picha: Ashraf Amr/AA/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limefahamisha kuwa msaada muhimu wa kibinadamu kwa Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha mpakani cha Rafah, hautasafirishwa leo Ijumaa kutokana na kukatika kwa huduma za mawasiliano ya simu.

Shirika la mawasiliano huko Palestina lilifunga hapo jana mitandao yote ya simu na intaneti kutokana na ukosefu wa mafuta kwenye ukanda huo.

Soma pia:Palestina yahofia maisha ya walionasa hospitali ya Al-Shifa 

Juliette Touma, mkurugenzi wa mawasiliano wa shirika la UNRWA, amewaambia waandishi wa habari huko Amman, Jordan kwamba wanashuhudia vitendo vya kutumia nishati ya mafuta, chakula, maji na misaada ya kibinadamu kama silaha ya vita.

Nahostkonflikt | Al-Schifa Krankenhaus in Gaza Stadt
Wapalestina wakiishi nje ya hospitali ya al-shifa huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel (12.11.2023)Picha: Ahmed El Mokhallalati/REUTERS

Touma amesema UNRWA haiwezi kufanya kazi kwa sababu haina mafuta, na kwamba inaghadhabisha kuona mashirika ya kibinadamu yamegeuzwa kuwa omba omba wa mafuta.

Mkurugenzi huyo wa UNRWA amesema Israel iliwapatia kiwango kidogo cha mafuta wiki hii kwa ajili ya kusambaza misaada ya chakula na hakuna miundombinu mingine, kama hospitali au mitambo ya usambazaji wa maji iliyoruhusiwa kutumia mafuta hayo.

Mapigano yaendelea Gaza na Jenin

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetangaza hii leo kwamba limefanikiwa kuichukua maiti ya mwanajeshi wake Noa Marciano, aliyekuwa ameshikiliwa mateka na baadaye kuuawa na kundi la wanamgambo wa Hamas. IDF imesema mwili wa mwanajeshi huyo ulipatikana katika  hospitali ya al-Shifa.

Hamas, ambayo inazingatiwa kuwa kundi la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa mengine, imedai kuwa mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 19 aliuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Moschee in Dschenin von israelischem Luftangriff getroffen
Raia wa Palestina wakiondoa vifusi katika msikiti baada ya shambulio la anga la Israel katika kambi ya wakimbizi huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. (22.10.2023)Picha: Raneen Sawafta/Reuters

Mapigano yameendelea huko Gaza na kwengine. Leo hii jeshi la Israel limesema limewaua watu watano inaodai kuwa ni "magaidi" katika kambi ya wakimbizi hukio Jenin kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Hamas ikikiri kuwa idadi kadhaa ya wapiganaji wake waliuawa katika shambulio hilo la usiku wa kuamkia leo.

Wapalestina waliolazimika kuondoka eneo la Kaskazini na kuelekea kusini, sasa wanakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu, hasa nguo na mablanketi katika msimu huu wa baridi.

"Ninaumia moyoni ninapowaona watoto wangu wakiwa kwenye baridi barabarani wakiwa wamevaa mashati ya mikono mifupi, ninaumia moyoni ninapowaona wakiwa  wakivaa nguo fupi na kukohoa. Hakuna mtu anayetusaidia, hakuna nchi inayotusaidia, " amesema Walid Osama Subh.

Mzozo huu kati ya Israel na Hamas tayari umesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 11,400 huku theluthi mbili miongoni mwa hao wakiwa ni wanawake na watoto. Hayo ni kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina inayodhibitiwa na Hamas. Upande wa Israel watu 1,200 waliuawa na wengine zaidi ya 200 walichukuliwa mateka.