1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UGONJWA WA USUBI UNGALI UKISAMBAA

chbuke16 Desemba 2006

MATIBABU YAKE NI RAHISI LAKINI UNASABABISHA MADHARA MAKUBWA

https://p.dw.com/p/CHlr

Nchi zaidi ya 35 zilizo kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa usubi zimehimizwa kuongeza kasi ya kupambana na ugonjwa huo ili kuweza kuutokomeza.

Hii ni pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuzuia, kutibu na kuwahamasisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo ambayo yanashambuliwa na ugonjwa huu wachukue tahadhari ikiwa ni pamoja na kumeza dawa za kuzuia ugonjwa huu na mapema.

Mkutano huu kwa upande mwingine ulionesha utashi mkubwa wa kisiasa kutokana na kuwa hata watawala na wanasiasa walihudhuria na kutoa ahadi za kuendeleza mapambano dhidi ya adui usubi.

Ndio maana mkutano huo ukawaleta kwa pamoja mabingwa kutoka sekta za afya kutoka nchi mbalimbali, zaidi ya mawaziri 20, wasomi na wanasiasa kutoka zaidi ya nchi 25 zilizo kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania binafsi ndiye aliufungua mkutano huo uliofanyika mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2006, naye akianisha madhara ambayo tayari yamesababishwa na ugonjwa huu kwa baadhi ya watanzania.

Kwa mujibu wa takwimu za mabingwa wa afya kwenye mkutano huo tayari mataifa 35, yanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Mataifa 28 kati ya hayo ni ya ki-Afrika. Jumla ya watu wanaougua ugonjwa huo kote ulimwenguni hivi sasa wamefikia milioni 18.

Ugonjwa huu hutokana na minyoo aina ya onchecerca volvulus na kusambazwa na inzi weusi majike wadogo-wadogo mithiri ya mbu wajulikanao kama simulium. Mbu hawa huzaliana kwa wingi kwenye maeneo yenye vijito au mito yenye maji yatiririkayo kwa kasi.

Wadudu hawa wana uwezo wa kuruka hadi umbali wa kilometa 400. Waziri wa Afya wa Tanzania na maendeleo ya Jamii Profesa David Mwakyusa anasema licha ya kuwa wadudu hawa wana umbo linaloshabiriana sana na la mbu lakini tabia zao ni tofauti kabisa.

“Kwa sababu wao wanapendelea kuzaa kwenye miamba ambapo kuna maji yanapita haraka.

Ambapo hawa mbu wanaoeneza malaria kama unavyojua wanatafuta maji ambayo yametuama kwa hiyo katika maeneo ambayo kuna mito ambayo ina maji ambayo yana kwenda haraka ndo unawapata”. Anasema waziri na kuyataja maeneo ambayo wanapatikana wadudu hawa sakili kwa hapa Tanzania kuwa ni kwenye mikoa ya Tanga, na Morogoro.

Akizungumza na idhaa hii Waziri huyo alionya kuwa hali ya kusambaa ugonjwa huu inazidi kuwa kitisho na kuwa matokeo yake badhi ya watu wameanza kuhama maeneo yao hali anayodai inarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi Tanzania.

Waziri anadokeza kuwa licha ya tatizo hilo kuongezeka Tanzania halijafikia kiwango cha baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.

“It is the disease of the pure” anasema waziri kwa lugha ya kiingereza akimaanisha kuwa ni ugonjwa wa watu maskini, na kuongeza. “ kwa hiyo unaanza kuwa na uchumi ambao ni hafifu halafu ukiongeza na matatizo kama hayo ndio unazidi na kama nilivyo eleza kwenye hotuba yangu tunayajua maeneo ambayo watu walikuwa wanalima lakini kwa sababu mito waliyokuwa wanaitumia ina mbu wengi hao na wao wamegundua kuwa hiyo ndio inatuletea upofu basi wanahama”.

Wataalamu katika mkutano huu wa Dar es salaam kwa pamoja walisisitiza umuhimu wa kupambana na ugonjwa huu kwa ushirikiano wa nchi zote zilizo katika mapambano au jirani ili kwa pamoja waweke kuweka mikakati ya kutokomeza adui usubi.

Hii bila shaka inatokana na ukweli kuwa ikiwa nchi moja itafanya juhudi za peke yake hata nchi hiyo ikifanikiwa yanaweza yasiwe mafanikio ya kudumu kwani ugonjwa huo unaweza kuingizwa tena kutoka nchi nyingine.

Mfano kamili ni nchi ya Kenya ambayo inadai iliteketeza ugonwa huu taklibani miaka 50 iliyopita lakini hivi sasa ugonjwa huo unatishia kurudi nchini humo kutokana na ujiro wa wakimbizi.

Hivyo ndivyo Dr. David Sam alivyoiambia Deutsche Welle alipokuwa akielezea hali ya ugonjwa wa usubi nchni Kenya.

Hata hivyo Dk. Sam anasema juhudi zinazofanywa na nchi yake ni kuhakikisha ugonjwa huo hausambai tena kwa wananchi. “ Tumejaribu kuzuia hao sisi sana kwa raiyaa lakini mahali refugee wako sio rahisi kusambaza huo ugonjwa”.

Njia inayopendekezwa na wataalamu katika kudhibiti ugonjwa huu ni kuwapa watu wote walio kwenye maeneo wanapopatikana wadudu hawa dawa ya kutibu na kuzuia usubi.

Waziri Mwakyusa anasema hii ndiyo njia rahisi ya kupambana na hali hii hasa ikilinganishwa na ikiwa serikali ingeamua kumpima kila mtu ili wapatikane watu wenye vijidudu vya usubi na kasha wapewe dawa.

Na tena njia hii inafikiriwa kuwa bora kwani dawa hizi hazimdhuru mtu ambaye labda amezimeza wakati hana vijidudu vya usubi.

“ Kwa hiyo tunachofanya katika maeneo ambayo tunajua kuna huo ugonjwa tunawapa dawa mara moja kila mwaka” anasema waziri Mwakyusa na kuongeza.

“katika kila mwaka kuna tarehe ambayo tumeweka. Tunajua wanakuja wote, wanapewa watu wote wadogo kwa wakubwa, tunarudi tena mwaka kesho kwa miaka mitatu mfululizo. Tegemeo lote ni kuwa tutakuwa tumemaliza baada ya kufanya hivyo”.

Mkutano huu wa Dar es salaam Joint action forum, ni wa 12 kwa maana maana mikutano kama hii imekuwa ikifanyika na kupitisha maadhimio. Swaku ambalo mtu anaweza kujiuliza ni mafanikio gani ambayo yamefikiwa? Waandishi wa habari walimuuliza waziri Mwakyusa ambaye anajibu.

“ Kwanza umoja wenyewe ni …..wa family moja wenye matatizo mamoja, tumekuja pamoja. programu hii ilianza Afrika magharibi na nchi zipataozo 11 tu.

Lakini kama ulivyosikia leo hii hapa tupo 36 kwa hiyo watu wakigundua na wenyewe wanajiunga tunabadilishana nao mawazo”.

Binafsi nilimuuliza Waziri Mwandosya kuwa ikiwa inajulikana wazi kuwa wadudu hao ndio hueneza usubi kuna juhudi zozote za kujaribu kuteketeza nzi hao naye akajibu “ Ndio na hapana. Huko tulipoanza mimi nikiwa bado mwanafunzi tulikuwa tunapiga spray ya dawa kwenye mito lakini unajua hiyo ni ngumu sana umetia dawa ya kutosha dawa inakwenda.

Kwa hiyo tukaona kwamba njia ambayo ni rahisi zaidi ni kuviua hivi vijidudu visiwepo kabisa.

Manake huyu mbu akikuuma hatapata kitu.

Tunaweza tukafanya lakini unaangalia kitu kinaitwa cost effectiveness unapotia hela kiasi hiki, unavuna kiasi gani kutumia mpango tofauti” anajibu waziri Mwandosya.

Wataalamu wanasema kuwa tangu mtu anapoumwa mbu mwenye vimelea vya ugonjwa huo hadi ugonjwa huo kujitokeza inachukua muda wa tangu mwaka mmoja hadi miwili.

Katika kongamano hilo aliletwa Bi Miriana Fernand. Mwanamama huyo alishambuliwa na ugonjwa huo kwa miaka mingi na kila mara alipobeba mamba ilitoka. Afya yake kwa ujumla ilizorota. Baada ya kupata matibabu hivi sasa amepona na tayari ana mtoto mwenye umri wa mwaka 1 na nusu.

Mama huyu aliwaonyesha waandishi wa habari sehemu ya miguu yake. Ingali na madoa kama ya chui licha ya kuwa yeye anadai madoa hayo yamepungua baada ya kupatiwa tiba.

Dalili za ugonjwa huu hujitokeza kwa binadamu katika sura 3 tofauti.

Kwanza ni kwenye ngozi ambayo huwasha sana, hupata upele na ukurutu , huvimba na kuwa kama ya mtu mwenye ukoma, hukakamaa na kuwa ngumu , huchakaa na kulegea, ngozi huwa na madoa madoa kama chui, ngozi huota vinundu. Kwenye mwili na ubongo kwa wagonjwa wachache ukuaji wa mwili na ubongo huathirika na kusababisha kudumaa vile vile kifafa kinaweza kutokea.

Kwenye macho mazalia ya filarial hudhuru macho na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kuona na hatimaye kusababisha upofu.

Takwimu za shirila ka Afya Ulimwenguni zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 85 wapo kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo katika nchi 27 za bara la Africa na nchi 6 za bara la Amerika ya kati ya Kusini.

Watu milioni 18 wamekwishia kuabukizwa kati yao watu milioni 1 wana shida ya kuona, na zaidi ya laki 4 wana upofu.

Hapa nchini Tanzania watu milioni 4 wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu katika mikoa ya Ruvuma, wilaya zote, Morogoro; wilaya zote, iringa ; wilaya ya Ludewa na maeneo mengie yatachunguzwa. Tanga; wilaya za Korogwe, Lushoto na Muheza Mbeya ; wilaya za Rungwe na Kyela.

Mpango wa kudhibiti ugonjwa huo nchini Tanzania ujulikanao kama National Onchocerciasis Controal Programme NOCP ulizinduliwa rasmi mwaka 1998 na unaendeshwa na wizara ya Afya chini ya Idara ya kinga.

Muundo wa NOCP unaenda sambamba na muundo wa mabadiliko ya sekta ya afya Health Sector Reform katika ngazi ya Taifa kuna kamati maalumu ya kudhibiti ugonjwa wa usubi, National Onchecerciasis Task Force NOTF ambayo majuku mu yake makubwa ni kufuatilia utendaji wa kazi zote zinazohusu udhibiti wa ugonjwa wa usubi nchini.

Dawa ambayo inatumika kutibu ugonjwa huu na iliyopigiwa sana upatu ni ile iitwayo mectizan ambayo hupewa mtu mara moja kwa mwaka kwa kipindi kisichopungua miaka 15 mfululizo.

Mwisho.