Ugiriki haina budi kukaza mkaja
30 Aprili 2010Kuambatana na masharti ya msaada wa kimataifa wa mabilioni ya Euro, hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni kupunguza mishahara na nafasi za ajira serikalini, kutotoa nyongeza ya mishahara kwa angalao miaka mitatu ijayo,kupandisha kodi ya mapato na mauzo. Hiyo imetangazwa kufuatia mkutano wa dharura uliofanywa mjini Athens kati ya Waziri Mkuu George Papandreou na vyama vya wafanyakazi na wafanyabiashara. Hatua hizo zinapingwa vikali na wananchi wengi na hiyo jana, ghasia zilizuka mjini Athens. Polisi ilitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliojaribu kuvamia jengo la wizara ya fedha.
Mpango huo wa kukaza mkaja, huenda ukawa mfano wa kufuatwa na nchi zingine za Ulaya ambazo vile vile zinapambana na matatizo makubwa ya deni. Kwani baada ya Ureno na Uhispania kuorodheshwa kama nchi zisizo na uwezo mzuri wa kulipa madeni yake, serikali za nchi hizo zinajitahidi kurejesha imani katika masoko ya fedha.
Mwandishi:P.Martin/DPA