1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugaidi si tishio kubwa Ulaya kama inavyodaiwa.

Omar Babu19 Aprili 2007

Wakazi wa Ulaya walipigwa na bumbuazi pale miji ya Madrid na London ilipokumbwa na mashambulizi ya kigaidi mwaka 2004 na 2005. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi karibuni wa shirika la polisi la Ulaya, Europol, unaonyesha kwamba hakuna uwezekano mkubwa kwa wakazi wa bara la Ulaya kuathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi kama inavyodaiwa.

https://p.dw.com/p/CHlB
Bendera ya Umoja wa Ulaya.
Bendera ya Umoja wa Ulaya.Picha: PA/dpa

Shirika la Europol limeorodhesha visa mia nne na tisini na nane vya kigaidi vilivyotokea katika mataifa ya muungano wa Ulaya mwaka jana na likasema kwamba visa vingi havikulengwa kuua.

Hata baada ya matokeo ya uchunguzi huo, taasisi nyingi za mataifa ya Ulaya zingali zikiwasumbua washukiwa na kukiuka haki za kibinadamu kwa visingizio vya kukabiliana na ugaidi.

Ujerumani, ambayo ndio inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya, inapanga kuzishawishi nchi 27 wanachama wa Umoja huo kuwa na utaratibu mpya wa kuhifadhi takwimu.

Waraka wa Ulaya wa mwaka 1950 kuhusu haki za kibinadamu unasisitiza haja ya kuheshimu taarifa za kibinafsi za mtu.

Ingawa hapo awali Tume ya Ulaya ilikuwa imependekeza kuwepo kwa kanuni za wazi kuhusu kutoa taarifa za washukiwa, Ujerumani inapendekeza Umoja wa Ulaya uwe huru kushauriana na mataifa mengine ambayo hayana utaratibu wa kuweka takwimu sawa na Muungano wa Ulaya.

Hoja hii hasa imezingatia mashauriano yanayoendelea kuhusu utaratibu wa muda mrefu wa kutoa taarifa wasafiri wa ndege kati ya Ulaya na Marekani.

Utaratibu huo utachukua mahali pa mwafaka wa muda uliotiwa saini kati ya Marekani na Muungano wa Ulaya mwaka uliopita.

Mwafaka huo wa mwaka uliopita ulitayarishwa baada ya Mahakama kuu ya Ulaya kuukosoa mwafaka kama huo uliotiwa saini mwaka 2004.

Wanaharakati wa kutetea raia wanadai hakuna uhakika wowote kwamba Marekani haitazitumia vibaya taarifa za raia wa Ulaya pindi zitakapotolewa.

Tangu mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani, serikali hiyo imeviagiza vyombo vyake vyote vya usalama kuchukua taarifa za watu wote wanaoingia nchini humo.

Mbunge wa chama Uholanzi katika bunge la Ulaya, Kathalijne Buitenweg, amesema hawatarajii mataifa yanayoendelea kuwa na uwezo sawa na Ulaya kuhifadhi taarifa za raia zao.

Profesa wa Kituo cha Haki za Binadamu katika Chuo Kikuu cha Essex, Steve Peers amesema mapendekezo ya Ujerumani yatavuruga usimamizi wa taarifa za mataifa yasiyokuwa ya Muungano wa Ulaya.

Kwa mujibu wa Profesa Steve Peers mapendekezo ya Ujerumani pia yanapunguza sio tu haki ya raia kujua taarifa ambazo zinashughulikiwa na serikali, bali pia fursa ya raia hao kujua taarifa zao zisizo sahihi.

Profesa Steve Peers anasema iwapo mapendekezo ya Ujerumani yatazingatiwa, haki za kimsingi za binadamu zitakiukwa kwa kiasi kikubwa.

Mwafaka wa kubadilishana taarifa ni moja wapo wa mbinu zilizolengwa kudhibiti ugaidi.

Mapema mwaka huu, Tume ya Ulaya ilipendekeza kuanzishwa mradi wa kuhakikisha alama za vidole vya raia wote wa Mataifa ya Umoja wa Ulaya zinahifadhiwa kabla ya mwisho wa mwaka 2008.

Hatua hiyo ilikabiliwa na upinzani mkali.

Bunge la Ulaya litakuwa na kikao mjini Strasbourg, Ufaransa kuanzia tarehe 23 hadi 26 mwezi huu.

Bunge hilo linatarajiwa kuzingatia kanuni zitakazoruhusu mataifa ya Ulaya kutumia ndege za ulinzi kuandamana na ndege za abiria zinazotoka katika mataifa ya Ulaya.

Mashirika ya ndege ya India na Israil yamekuwa yakitumia ndege za ulinzi kuandamana na ndege za abiria.

Mbunge wa Italia wa Umoja wa Ulaya, Paolo Costa, aliyetayarisha mswada wa msimamo wa bunge kuhusu kanuni hizo mpya, amesema hatimaye itakuwa jukumu la mataifa husika kuamua endapo watatumia ndege za ulinzi kulingana na sheria zao za ndani.