1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugaidi ni kitisho kwa wote

P.Martin9 Agosti 2007

Viongozi wa kisiasa na wa makundi ya kikabila kutoka Afghanistan na Pakistan wanakutana katika mji mkuu wa Afghanistan,Kabul katika juhudi za kutafuta amani.

https://p.dw.com/p/CB24
Wanamgambo wa Taliban wakidhibiti barabara ya Kandahar kuelekea Herat nchini Afghanistan
Wanamgambo wa Taliban wakidhibiti barabara ya Kandahar kuelekea Herat nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/dpa

Mada kuu ya mkutano huo inahusika na suala la usalama,hasa katika maeneo ya mpakani yanayodhibitiwa na Wataliban.

Hali ya usalama imeimarishwa mjini Kabul,ambako Jirga au Baraza la zaidi ya wajumbe 700 kutoka Afghanistan na Pakistan linakutana chini ya ulinzi wa askari polisi 2,500

Pakistan inawakilishwa katika mkutano huo wa siku tatu na Waziri Mkuu Shaukat Aziz,baada ya Rais Pervez Musharraf kuamua dakika ya mwisho kutokwenda mkutanoni.Aziz amefuatana na kiasi ya wajumbe 175 kutoka serikalini na makundi ya kikabila.

Makubaliano ya kuitisha mkutano huu yalipatikana mwishoni mwa mwaka uliopita mjini Washington,kati ya Rais wa Afghanistan Hamid Karzai na Rais Musharraf wa Pakistan.Azma ni kwa Pakistan na Afghanistan zinazozana mara kwa mara,kutafuta njia ya kupigana pamoja dhidi ya Al-Qaeda na Taliban.

Rais Karzai alipoufungua mkutano hii leo alisema, ana hakika na imani,kuwa inawezekana kuyateketeza makundi hayo mara moja,kama watakuwa na azma moja.Akaongezea,ni matumaini ya wananchi wa Afghanistan na ndugu wa Pakistan kuwa mkutano huu wa amani utafanikiwa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Pakistan Shaukat Aziz amesema,hatima za watu wa Pakistan na Afghanistan zimefungamana:vile vile Pakistan wala haina lengo la kuidhibiti Afghanistan ili kutumikia maslahi yake.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usalama wa Afghanistan Haroun Mir,ni muhimu kwa Pakistan na Afghanistan kuwa na mkakati mmoja wakati huu ambapo mashambulizi ya Taliban na Al-Qaeda yanaziidi kushika kasi.

Akasema,wanachokitaka mwishoni mwa mkutano huu wa Jirga,ni kwa raia wa Afghanistan na Pakistan kuelewa kwamba ugaidi ni kitisho kilicho adui wa nchi zote mbili.

Mara kwa mara,Afghanistan huituhumu Pakistan kuwa inawahifadhi wanamgambo wa Taliban na Al-Qaeda kwa azma ya kuidhoofisha nchi ya jirani.

Pakistan lakini inakanusha madai hayo,ikisema imeshawakamata viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa Al-Qaeda na vile vile,inapambana na kitisho cha Wataliban katika maeneo ya kikabila kwenye mpaka wa Afghanistan unaogombewa.

Wanamgambo wameimarisha mashambulizi yao ndani ya mpaka wa Pakistan hasa katika eneo la kaskazini-magharibi,tangu vikosi vya serikali kuvamia Msikiti Mwekundu mjini Islamabad.

Watu 102 waliuawa katika shambulizi hilo,mwezi uliopita.Mashambulizi ya mpakani nayo yamesababisha zaidi ya vifo 200.