1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yataka mkataba wa Iran kudumishwa

Lilian Mtono
19 Septemba 2017

Ufaransa imetoa wito mpya kwa Marekani juu ya kuendelea kuwepo kwa mkataba wa nyuklia wa Iran, katika makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015

https://p.dw.com/p/2kJKU
New York Emmanuel Macron, Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Ufaransa pia imependekeza kuwa baadhi ya vipengele katika mkataba huo unavyoelekea kumalizika muda wake kwamba vinaweza kuimarishwa wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump ameukosoa kwa mara nyingine mkataba huo kwa kusema una makosa mengi. 

Mkataba kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu zaidi duniani, ulioitaka Iran kupunguza mpango wake wa nyuklia ili iweze kupatiwa nafuu ya vikwazo vya kiuchumi unakabiliwa na kitisho wakati ambapo Rais Trump atakapoamua ifikapo Oktoba 15 iwapo atathibitisha kama Iran inatimiza masharti ya makubaliano hayo.

Iwapo Trump, ambaye hadi wiki iliyopita aliituhumu Iran kwa kukiuka mambo muhimu kwenye mkataba huo ataamua kutothibitisha mkataba huo unaweza kubatilishwa, na kuchochea mzozo wa kikanda. Trump ambaye ameyataja makubaliano hayo yaliyofikiwa wakati wa utawala wa mtangulizi wake Barack Obama kuwa makubaliano mabaya zaidi kuwahi kufikiwa hajaficha maoni yake kuhusu suala hilo la Iran alipokutana na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Brian Hook mkurugenzi wa sera za mipango katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema Rais Trump anaamini mpango huo ujulikanao mpango madhubuti wa pamoja kuhusu Iran JCPOA una mapungufu makubwa na alimuelezea Rais Macron kuhusu mtizamo wake kuhusu mapungufu hayo.

Hook amesema viongozi hao wawili pia walijadili mkakati wa pamoja dhidi ya Iran ambao utazingatia kile kinachotajwa kuwa msimamo wa Iran kuunga mkono ugaidi, mpango wake wa kinyuklia, mchango wake katika msukosuko unaojiri katika kanda ya Mashariki ya Kati miongoni mwa vitendo vyake vingine vya kichochezi.

Alipoulizwa na wanahabari iwapo ataheshimu makubaliano yaliyofikiwa kuhusu Iran, Trump aliwaambia aliyekuwa anakutana na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumatatu alisema hivi karibuni watapata majibu .Maafisa wa Israel wamesema wanataka makubaliano hayo ya JCPOA kuhusisha kurefushwa kwa muda wa kusitishwa kwa mpango wa kinyuklia wa Iran ambao ni miaka kumi na hata ikiwezekana kuusitisha kabisa badala ya kusitisha tu operesheni zake.

USA Präsident Ruhani im CNN Interview Screenshot
Iran ilifikia makubaliano ya nyuklia na mataifa sita yenye nguvu dunianiPicha: CNN

Makubaliano hayo kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran ulifikiwa kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu zaidi duniani Marekani, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Nchi hizo sita zitakutana kesho Jumatano na Iran katika ngazi ya mkutano wa mawaziri. 

Uwezekano wa Marekani kubadilisha msimamo wake kuhusu makubaliano hayo, kumewafanya baadhi ya washirika wake ambao walichangia katika kufikiwa kwa makubaliano hayo kuwa na wasiwasi hasa wakati huu ambao kuna mzozo mwingine unaohusiana na mpango wa kinyukliwa wa Korea Kaskazini ambayo imekuwa ikifanyia majaribio mpango wake wa kinyuklia na kurusha makombora.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesema ni muhimu kudumisha makubaliano hayo ili kuepusha utapakaaji wa silaha za kinyuklia hasa wakati huu ambapo kuna kitisho pia kutoka kwa Korea Kaskazini na kuongeza Ufaransa itajabribu kumshawishi Rais Trump kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kudumisha makubaliano hayo ya Iran hata kama kutakuwa na haja ya kuutathmini upya baada ya mwaka 2025.

Iwapo Trump hatathibitisha kuwa Iran inaheshimu makubaliano hayo, bunge la Marekani litakuwa na siku 60 kuamua iwapo itarejesha vikwazo dhidi ya Iran ambavyo vilikuwa vimeondolewa chini ya makubaliano hayo yaliyofikiwa 2015. Kiongozi wa kidini wa Iran mwenye ushawishi Ayatollah Ali Khemenei ameonya kuwa Iran itajibu vikali hatua yoyote ambayo inaendana kinyume na makubaliano hayo kutoka kwa Marekani.

Ufaransa ilikuwa mojawapo ya nchi ambazo zilikuwa na msimamo mkali dhidi ya Iran katika mazungumzo ya kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kinyuklia lakini imekuwa mwepesi kurejesha mahusiano ya kibiashara na Marcron amesema mara kwa mara kuwa hakuna njia mbadala kuhusu makubaliano hayo na kwamba  Shirika la Kimataifa  la nguvu za Atomiki -IAEA halijatoa tamko kukinzana na mtizamo wa Ufaransa. Maafisa wa Ufaransa wamesema Iran inaheshimu makubaliano yaliyofikiwa.

Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba