Ufaransa yalitaka Baraza la Kijeshi Misri kuachia madaraka | Matukio ya Afrika | DW | 19.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Ufaransa yalitaka Baraza la Kijeshi Misri kuachia madaraka

Mahakama ya Misri imeahirisha uamuzi wa kukipiga marufuku chama cha Udugu wa Kiislamu, huku Ufaransa ikilitaka Baraza la Kijeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo na maandamano yakipamba moto.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.

Hali nchini Misri inaelezwa kuwa ya wasiwasi na mashaka, huku watu wakiendelea kumiminika katika uwanja wa Tahrir kwa ajili ya maandamano makubwa, ambayo yanaungwa mkono kikamilifu na chama cha Udugu wa Kiislamu.

Mwandishi wa Deutsche Welle aliye mjini Cairo ameelezea kushuhudia misururu ya watu ikishuka kwenye uwanja huo, ingawa amesema hali ya joto kali huenda ikayafanya maandamano kuanza rasmi saa za jioni baada ya jua kutua.

Timu ya kampeni ya chama cha Udugu wa Kiislamu, ambayo inadai mgombea wao Mohammed Mursi kuwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi mwishoni mwa juma, imesema inashirikiana na makundi kadhaa katika maandamano yanayoanza leo, kupinga tangazo la baraza la kijeshi linalotaka kuyakata madaraka ya raisi ajaye wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa timu hiyo, maandamano hayo pia ni kupinga tangazo uamuzi wa mahakama ya katiba, ambayo wiki iliyopita ililivunja bunge la nchi hiyo linalotawaliwa na vyama vyenye msimamo wa kidini.

Moja wapo ya makundi ya vijana yaliyoshiriki kwenye mapinduzi ya umma ya Februari 2011, linaloitwa Aprili 6, limesema kuwa linashiriki kwenye maandamano ya leo.

Kesi dhidi ya Udugu wa Kiislamu yaahirishwa

Waandamanaji wakichoma picha ya Ahmed Shafiq.

Waandamanaji wakichoma picha ya Ahmed Shafiq.

Maandamano ya leo yanafanyika huku mahakama nchini humo ikiahirisha kesi inayotaka kufutwa kwa kundi la Udugu wa Kiislamu, hadi hapo Septemba Mosi.

Kwa mujibu wa chanzo cha mahakama hiyo, aliyepeleka ombi hilo ni mwanaharakati na mwanasheria Shehata Mohammed Shehata, akiutuhumu Udugu wa Kiislamu kwa kuvunja sheria inayotaka asasi za kiraia kujisajili kwa mamlaka za seriali na iliyowapiga marufuku kushiriki siasa.

Kundi la Udugu wa Kiislamu lililoanzishwa mwaka 1928 limekuwa na nguvu kubwa kisiasa nchini Misri kwa muda mrefu sasa. Lilipigwa marufuku rasmi wakati wa utawala wa Hosni Mubarak, lakini kimsingi lilikubaliwa kufanya kazi zake kwa masharti maalum.

Baada ya mapinduzi ya umma yaliyomuondoa madarakani Mubarak hapo mwaka 2011, Udugu wa Kiislamu ulianzisha chama cha kisiasa cha Uhuru na Haki ambacho kilijizolea nusu ya viti katika uchaguzi wa bunge.

Katika uchaguzi wa uraisi, chama hicho kilimsimamisha mhahdiri wa zamani wa chuo kikuu, Mohammed Mursi, ambaye matokeo yasiyo rasmi yaliyotolewa na vyombo vya habari, yanaonesha kuwa huenda akatangazwa mshindi, wakati matokeo rasmi yatakapotolewa hapo Alhamis.

Shafiq adai kushinda

Mgombea wa Udugu wa Kiislamu, Muhammed Mursi.

Mgombea wa Udugu wa Kiislamu, Muhammed Mursi.

Hata hivyo, tayari meneja kampeni wa mpinzani wa Mursi kwenye uchaguzi huo, Ahmed Sarhan, amesema kwamba mgombea wake Ahmed Shafiq ndiye aliyeshinda kwa asilimia 51 ya kura.

Kesi hii dhidi ya Udugu wa Kiislamu imekuja baada ya kesi nyengine ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa bunge kushinda na kupelekea bunge zima kuvunjwa na mahakama ya Katiba mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika hatua nyengine, Ufaransa imeungana na Marekani na Ujerumani kupaza sauti zao dhidi ya kile kinachoonekana kama nia ya jeshi nchini Misri kusalia madarakani, hata baada ya uchaguzi wa rais.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, Bernard Valero, amewaambia waandishi wa habari hivi leo kwamba jeshi la Misri linapaswa kurejesha utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza