1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa baada ya uchaguzi wa rais

Oummilkheir8 Mei 2007

Machafuko yameripotiwa katika sehemu mbali mbali nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/CHEh
Picha: AP

Waandamanaji waliokusanyika katika uwanja mashuhuri wa Bastille mjini Paris waliongozana milango ya saa tatu za usiku hadi katika uwanja wa Voltaire-mtaa wa 11,wakipaza sauti “Sarko Fashisti,wananchi watakupata tuu huku wengine wakihanikiza kwa makelele mfano Paris simama imara,zindukana.”

Majiani waandamanaji hao walitia moto piki piki moja na kuvunja madirisha ya viyoo ya maduka kadhaa,vibanda vya simu na kuharibu magari ya watu pia.Vikosi maalum vya usalama CRS vimejaribu kuwazuwia waandamanaji wasisonge mbele-uamuzi uliochukua sura ya watu kufukuzana kati ya uwanja wa Bastille na ule wa Republique kupitia njia zinazoelekea Belleville.

Saa moja baadae,milango ya saa nne za usiku waandamanaji walitawanyika kwa makundi madogo madogo wakiwakimbia polisi.

Saa tano za usiku kundi jengine la vijana wasiopungua mia tatu walimiminika tena katika uwanja wa Bastille na kujarkibu kuzuwia shughuli za usafiri.Zaidi ya waandamanaji mia moja wamekamatwa mjini Paris.

Mjini Nantes,kaskazini magharibi ya Ufaransa ,waandamanaji zaidi ya 400 ambao polisi wanasema ni wafuasi wa siasa kali za mrengo wa shoto walikusanyika pia jana usiku katika uwanja mkuu wa mji huo.Wametia moto magari na kuvunja viyoo vya jumba la mahakama.

Vikosi vya usalama vilivyotumia gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji hao,vimewatia mbaroni pia baadhi ya waandamanaji hao.Mjini Lyon pia kusini mwa Ufaransa sawa na Caen waandamanaji kati ya mia tano na mia nane waliteremka majiani kulalamika dhidi ya kuchaguliwa Nicolas Sarkory kua rais mpya wa Ufaransa.

Maaandamano yalianza tangu jana jioni ambapo wanafunzi kama300 wa shule za sekondari waliandamana katika uwanja wa Bastille dhidi ya mgombea wa chama cha UMP, Nicolas Sarkozy.

Makundi kadhaa ya mrengo wa shoto,likiwemo lile la mapinduzi ya kikoministi-LCR yaliwatolea mwito wafuasi wao wasimame kidete kupinga kuchaguliwa Nicolas Sarkozy-bila ya kutoa muongozo maalum wa maandamano hayo kwa siku zijazo.

“Baadhi ya wanaharakati wameteremka kwa mara ya tatu majiani-lakini hakuna muongozo kwa daraja ya taifa” amesema msemaji wa shirikisho la ajira CNT.

Machafuko yaliripuka takriban kote nchini Ufaransa usiku wa jumapili kuamkia jumatatu,mara baada ya Nicolas Sarkozy kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais.Magari 730 yalitiwa moto,askari polisi na gendarmes 78 walijeruhiwa na waandamanaji 592 kukamatwa.